AZAKI zitimize wajibu wake fedha za Mfuko wa Jimbo

28Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
AZAKI zitimize wajibu wake fedha za Mfuko wa Jimbo

MFUKO wa Maendeleo ya Jimbo la Uchaguzi (CDCF) ulianzishwa kwa Sheria ya Mfuko huo ya Mwaka 2009 kwa lengo la kuchochea maendeleo ya jimbo.

Sheria hiyo inahusu majimbo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, usimamizi na uangalizi wake ukiwa chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayesimamia Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, uko chini ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Masuala ya Muungano, akisaidiwa na maofisa waangalizi wa fedha zitakapokuwa zimetumwa kwenye majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Zanzibar.

Kulingana na matakwa ya kifungu cha 4(3) cha sheria ya mfuko huo, matumizi yote ya fedha kutoka kwenye mfuko yatapaswa kufanywa kulingana na matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2013 na Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo pamoja na kanuni zake.

Kifungu cha tano (5) cha Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Uchaguzi kinaelezea utaratibu utakaotumika katika kutenga fedha kwa ajili ya mfuko huu, pia taratibu za kufuatwa katika matumizi ya fedha hizo.

Huku kukiwapo taratibu za kuzingatiwa katika matumizi ya fedha, tayari kuna taarifa za matumizi mabaya ya fedha za mfuko huo katika baadhi ya maeneo nchini.

Mathalani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake ya mwaka 2019/20, alibainisha kuwapo shida kwenye matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo, baadhi zikitumika kutekeleza miradi ya vyama vya siasa na hata ya taasisi za dini isiyogusa wananchi moja kwa moja.

Hali hiyo sio tu kwamba ni matumizi mabaya ya fedha za umma, bali ni ishara ya kutokuwapo uwajibikaji miongoni mwa wanaopaswa kuusimamia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

Sehemu ya tatu ya Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo inaelezea uwapo wa kamati ya kusimamia fedha za mfuko, itakayokuwa na wajumbe wasiozidi saba wakiongozwa na mbunge aliyechaguliwa na wapigakura wa jimbo husika la uchaguzi.

Nipashe pia tunatambua kwamba vipo vifungu ndani ya sheria hiyo vinavyoainisha wajumbe wengine wa kamati hiyo, wakiwamo maofisa watendaji kata kwa Tanzania Bara na masheha kwa Tanzania Zanzibar.

Tunakumbusha kwamba sheria hiyo inaelekeza mjumbe mmoja atakayeteuliwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo kutoka kwa Asasi ya Kiraia (AZAKI) iliyo hai na inayoendesha shughuli zake kwenye jimbo husika la uchaguzi, pia utaratibu wa kumpata ambao hufanywa wakati wa kikao chake cha pili baada ya kamati kuzinduliwa na kuanza rasmi shughuli zake.

Kwa kuzingatia matakwa haya ya kisheria, Nipashe tunazikumbusha AZAKI kuhakikisha zinatekeleza wajibu huu kwenye usimamizi na uangalizi wa mfuko huu, ili kuongeza uwajibikaji na ulinzi wa fedha za umma.

Tunaamini AZAKI zikiwajibika vizuri katika hili, ni wazi maslahi ya wananchi wa jimbo la uchaguzi yatazingatiwa kwa kuhakikisha kunakuwapo na usimamizi bora na uwajibikaji stahiki katika matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo, ili kuwaletea wananchi maendeleo wanayostahili.

Mjumbe wa AZAKI katika kamati husika ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, anabeba wajibu mkubwa wa kuhakikisha fedha za mfuko zinatumika vizuri na kunakuwapo na thamani ya fedha kwa matumizi yote ya fedha za mfuko.

Nipashe tunaamini kwamba, kwa kufanya hivyo tu, kutakuwapo na maana ya uwapo wa mjumbe mwakilishi wa AZAKI katika jimbo la uchaguzi.

Habari Kubwa