Bomoabomoa aina hii iepukwe kuzuia hasara

12Mar 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Bomoabomoa aina hii iepukwe kuzuia hasara

VILIO vilitanda katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana wakati wa utekelezaji wa operesheni ya kubomoa nyumba zaidi ya 100 zinazodaiwa kujengwa kwenye eneo la reli ya kati.

Hasara iliyopatikana kwa wahusika ni kubwa. Hilo lilidhihirika wazi kutokana na ukweli kwamba nyumba nyingi zilikutwa na watu waliokuwa wakiendelea kuishi.

Hasara kubwa iliwakuta wengi pia kutokana na vitu vyao vya ndani kuharibiwa, baadhi vikiwa ni makochi, friji, vitanda, magodoro na hata vyombo vya kupikia.

Waathirika wengi walilalamikia operesheni hiyo. Kwamba, haikujali utu. Wengine walidai kuwa hawakupewa nafasi ya kuokoa mali zao. Wapo viongozi wa mtaa waliolalamikia pia jambo hilo, wakidai kwamba hawakushirikishwa katika utekelezaji wa operehseni hiyo.

Hata hivyo, wabomoaji ambao walitumwa na Shirika la Reli (TRL) linalomiliki eneo husika, walisisitiza kuwa operesheni hiyo imefanyika kwa usahihi hasa baada ya wahusika kuambiwa kitambo juu ya umuhimu wa kuondoka. Taarifa nyingine zilidai kuwa baadhi ya nyumba zilikuwamo katika orodha ya maeneo ambayo malipo yalishafanyika kitambo na hivyo wahusika kutakiwa waondoke.

Kwa ujumla, zipo taarifa tofauti kuelezea jambo hilo. Kila upande, kwa maana ya mamlaka zilizoamuru kubomolewa kwa nyumba hizo na wale walioathirika, wamekuwa na yao ya kueleza.

Sisi, Nipashe, siyo nia yetu kwa sasa kueleza ni nani walio sahihi. Ni imani yetu kuwa zipo mamlaka zinazoweza kufanya hivyo pindi ikibidi.

Hata hivyo, jambo muhimu tunalodhani kwamba ni vizuri likazingatiwa kupitia kadhia hii ni juu ya kuepuka namna ya ubomoaji uliofanyika jana.

Kile kilichoshuhudiwa hakipaswi kuachwa kitokee tena. Kubomolewa kwa nyumba zinazotumiwa kwa makazi ilhali baadhi ya wahusika wakiwa na vitu vyao ndani hakufai kujirudia. Sisi tunaona kuwa kufanya hivyo, ni sawa na kurudisha nyuma maendeleo.

Kwa mfano, vinaposambaratishwa vitu vya ndani, maana yake wahusika wanakumbwa na hasara mara mbili. Kwanza, ya kuharibiwa nyumba na pili, kuharibiwa kwa vitu hivyo vya ndani ambavyo baadhi watalazimika kuvuja jasho kwa miaka mingi ili kuvimiliki tena.

Aidha, upo uwezekano pia kwa baadhi ya waathirika kupoteza nyaraka zao muhimu. Vyeti vya kuzaliwa, vya shule, vitambulisho na hata madaftari ya shule ya watoto wao ni baadhi ya vitu vinavyoweza kuwa sehemu ya vile vilivyoharibiwa. Wengi wameumia.

Wanalia na kusaga meno kwa sababu siyo wote wanaoweza kuhimili pigo hili la aina yake katika maisha.

Kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa tukio hilo la Buguruni linapaswa kuwa somo kwa kila upande. Mamlaka zozote zile, iwe ni Serikali kuu, taasisi au halmashauri, zinapaswa kuangalia kwa kina juu ya athari za kuwabomolea watu nyumba zao kwa namna iliyoonekana jana. Ni vyema zifanyike jitihada za kila namna kuepusha ubomoaji wa aina hiyo.

Aidha, wananchi wanapaswa pia kuheshimu maamuzi halali ya mamlaka mbalimbali na kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao kwa haraka ili kujiweka mbali na hasara zinazoweza kuepukika.

Kubishana na mamlaka, au kuamini kuwa notisi inapotolewa huwa ni vitisho tu visivyo na utekelezaji, hakuna sababu. Ni kamari ya hatari

Kwa mfano, kama ni kweli kuna malipo stahili yalishafanyika kwa baadhi yao, ni wazi kwamba hakukuwa na haja ya kuendelea kubaki eneo hilo.

Shime, jambo hilo lililotokea Buguruni liwe funzo kwa kila mmoja. Jitihada zifanyike kungali mapema kuepuka ubomoaji unaohusisha nyumba zenye watu wanaoendelea kuishi ndani ili kuzuia hasara zinazoepukika.

Habari Kubwa