Bravo Msajili Vyama vya Siasa kwa ufafanuzi huu

13Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bravo Msajili Vyama vya Siasa kwa ufafanuzi huu

JUZI Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ali Ahmed, aliwatoa wasiwasi wadau wa siasa nchini na umma kwa ujumla, kwa kuvihakikishia vyama vya siasa kuwa hakuna kitakachofutwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Naibu Msajili huyo alifafanua kwamba sheria ya vyama vya siasa haimpi mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kufuta chama chochote kabla ya miezi 12 (yaani mwaka mmoja) kabla ya uchaguzi, na kama ingekuwa ni kufuta jambo hilo lingefanyika miezi 12 kabla ya Oktoba mwaka huu.

Ufafanuzi huu unakuja siku chache baada ya Ofisi ya Msajili kutangaza kuanza kufanya uhakiki wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu ambavyo ni 19.

Mambo yatakavyoangaliwa ni kama chama kina ofisi, mahesabu yake yako vizuri, kimesajiliwa na kadi za wanachama ziwe na picha zao.

Ofisi hiyo ilifafanua zaidi kuwa uhakiki huo unalenga kuwekana sawa na kama kutakuwa na kasoro, watapewa muda wa kujirekebisha, na kwamba jambo hilo halikuwa na lengo la kufuta chama na kwamba kama kutakuwa na kasoro, kutakuwa na muda wa kuzirekebisha kasoro hizo.

Aidha, alisema lengo ni kuhakikisha vyama vyote vya vinatulia na kukaa kwenye mstari kwa kuwa wakati wa Uchaguzi Mkuu watakuja waangalizi kutoka nje ambao watapita kwenye vyama.

Hizi zimekuwa habari njema kwa umma, wadau na vyama vya siasa, ambavyo baada ya kusikia habari hizo vilihisi kuwa lengo kuu la kufanya uhakiki ni kuvifuta na kuzua taharuki ikiwa imebaki miezi takribani saba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa na wadau walikuwa wanalalamika na kudai kuwa kuna nia ya kufuta vyama katika kipindi hiki ambavyo vyote vipo kwenye maandalizi ya kuelekea uchaguzi huo, ingawa hakukuwapo mamlaka ya serikali iliyokuwa imethibitisha taarifa hizo.

Kwa ujumla kitendo cha msajili kujitokeza hadharani na kutuliza hali ya wasiwasi iliyoanza kujitokeza kwenye vyama na wadau, ni cha kupongeza kwa kuwa sasa hali ya utulivu inakwenda kurejea miongoni mwao.

Ufafanuzi kama huu unahitajika pale linapotokea jambo linalogusa maslahi ya wengi kwenye jamii, ili kuondoa wasiwasi au namna yoyote ya kuwafanya watu wasitulie kutokana na kuwapo kwa taarifa potofu.

Vyama vingi kwa sasa akili ziko kwenye kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo vinapokumbana na vikwazo ambavyo ni tishio kwao wasiwasi unapandisha joto lao na kushindwa kufanya vyema kwenye shughuli zao za kisiasa.

Hatua ya Msajili kulitolea suala hilo ufafanuzi ina tija kwa sababu inarejesha imani ya vyama vya siasa, wadau na umma kwa ujumla kwa taasisi hiyo, ambayo ndiyo mlezi na msimamizi wa vyama vya siasa.

Pia inaweka mazingira ya kuvijengea imani vyama, wadau na umma kuelekea uchaguzi mkuu kwamba hakuna mamlaka yoyote ya serikali yenye nia mbaya ya kuvifuta bila kufuata taratibu za kisheria.

Sisi tunaona kuwa vyama vinapaswa kutoa ushirikiano kwa kujiweka sawa na uhakiki huo kwa kuwa umeeleza bayana mambo yatakayoangaliwa kwenye suala hilo, kwa kuwa lengo ni zuri la kuhakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992.

Ihakiki hio ni muhimu kwa kuwa kwa kipindi kirefu tumeshuhudia baadhi ya vyama vikishindwa kuzingatia sheria hiyo hususan kutokuwa na ofisi zinazoeleweka nchi nzima, wanachama na kutokufanya shughuli za kisiasa hadi wakati wa uchaguzi.

Ndio maana baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikiitwa ‘vyama vya uchaguzi’.

Habari Kubwa