Bravo NEC ushirikishaji wa wadau uboreshaji daftari

21Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bravo NEC ushirikishaji wa wadau uboreshaji daftari

MAANDALIZI ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, yameanza baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanza mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Maboresho ya daftari hilo yanatarajiwa kuanza mwezi ujao katika mikoa yote nchini, ambapo walengwa watakuwa ni wale waliopoteza kadi zao za kupigia kura, wapigakura wapya na waliohama maeneo yao. Uboreshaji wa daftari ni takwa la kisheria, ndio maana NEC imeanzisha mchakato huo.

Kumekuwapo na malalamiko mengi tangu daftari hilo lilipoanza kutumika mengi yakihusu wapigakura kutokukuta majina yao katika orodha ya wapigakura siku ya uchaguzi, hivyo wengi kukosa haki yao ya kupiga kura.

Hali hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wagombea, wapigakura, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, hivyo kutoa taswira mbaya ya NEC; kwamba inashindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kuratibu na kusimamia uchaguzi.

Lingine ambalo limekuwa likilalamikiwa ni uteuzi wa waandikishaji wa daftari na wasimamizi wa uchaguzi, kubwa likiwa ni kukosa imani na baadhi yao; kuwa wanapewa nafasi hizo kwa kuzingatia itikadi za vyama.

Hata hivyo, katika maandalizi ya uboreshaji wa daftari hilo, Tume imechukua hatua kadhaa, lengo likiwa kuepusha malalamiko na changamoto zingine.

Kikubwa ambacho NEC imekifanya, na ambacho kinastahili pongezi ni kushirikishaji wa makundi yote ya jamii kwa kuandaa semina na kujadiliana nayo kuhusiana na mambo mbalimbali, yakiwamo kueleza sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya tume kuhusiana na mchakato wa uboreshaji wa daftari hilo. Kwa kufanya hivyo, itapata mawazo na maoni tofauti yatakayoisaidia kuboresha utendaji.

Kwa kipindi cha wiki mbili hadi jana NEC ilikutana na kila kundi kwa siku moja jijini Dar es Salaam. Makundi yaliyohusishwa ni ya wadau kutoka vyama vya siasa; viongozi wa dini; wanawake, vijana na watu wenye ulemavu; vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Utaratibu huo ni mzuri kwa kuwa umewawezesha wadau kutoa maoni na mapendekezo yao pamoja na NEC kuwapa ufafanuzi wa sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji na uboreshaji wa daftari hilo.

Miongoni mwa mambo ya msingi na ambayo yatasaidia kuufanya mchakato wa uboreshaji kuwa na ufanisi na kupunguza malalamiko ya wadau ni NEC kuwa na ushirikiano wa karibu na wadau hususan vyama vya siasa.

Hii inatokana na kusisitiza kwamba itakahikisha vyama vyote vinapewa nakala ya daftari hilo baada ya kuhakikiwa pamoja na utaratibu wa kuvipatia nafasi ya kutoa maoni kuhusu majina ya maofisa wa uandikishaji baada ya kuteuliwa kwao.

Tunaamini pamoja na taratibu nyingine ambazo tume imeainisha kuzitumia kufanikisha mchakato huo ikiwamo kutumia vyombo vya habari, matangazo kupitia gari lake maalum litakalokuwa likipita maeneo mbalimbali nchini, semina na burudani, wananchi wengi watapata elimu na bila shaka lengo litafanikiwa.

Tunaamini kuwa asasi zilizopewa jukumu la kutoa elimu wakati huu wa uboreshaji daftari zitatekeleza jukumu hilo hilo kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na maelekezo yatakayotolewa na tume, huku tukitarajia vyama vya siasa ambavyo ni wadau wakuu wa uchaguzi kuwahimiza na kuwahamasisha wanachama wao wenye sifa za kuandikishwa wanachangamkia fursa hiyo.

Bila shaka walengwa ambao ni wenye akili timamu, uraia wa Tanzania na wenye umri kuanzia miaka 18, watajitokeza kwa wingi ili watumie haki yao ya kushiriki katika uchaguzi Oktoba mwakani.

Habari Kubwa