Bravo serikali, lakini bado kuna maswali

26Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bravo serikali, lakini bado kuna maswali

Serikali imetoa Waraka wa Elimu namba 2 mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji shuleni wa wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali.

Wanafunzi wanaohusika ni waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali kama utoro, utovu wa nidhani na kupata ujauzito, pia baadhi ya wanafunzi hushindwa kuhudhuria masomo kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kifamilia au wazazi kuhama maeneo bila kufuata taratibu za uhamisho wa watoto wao.

Aidha, utekelezaji wa waraka huo umeanza Novemba 24, mwaka huu, na umeangalia maeneo matano ambayo ni wanafunzi watakaokatiza masomo kutokana na ujauzito au utoro wataruhusiwa kurudi shuleni ndani ya miaka miwili tangu walipokatiza masomo.

Wakuu wa shule/walimu wakuu wahakikishe wanafunzi waliokatiza masomo na kurudi shuleni wanapata huduma za ushauri na unasihi ili kuwajenga kisaikolojia sambamba na wanafunzi wengine waliopo shuleni. Pia, wahakikishe mwanafunzi aliyekatiza masomo anarejea mwanzoni mwa mwaka wa masomo katika darasa alilokuwa anasoma.

Aidha, walimu wahakikishe mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji unafanyika katika mazingira bora kwa wanafunzi wote.

Pia, viongozi wa elimu katika ngazi zote wafuatilie na kutathmini utekelezaji wa waraka huo, huku mipaka ya waraka ikitajwa kuwa hautahusu wanafunzi waliofukuzwa shule kutokana na makosa yenye mawelekeo wa jina au mwenendo unaohatarisha amani shuleni, na kwamba watakaothibitika kutenda makosa hayo na kufukuzwa shule wanashauriwa kuendelea na masomo kupitia elimu nje ya mfumo rasmi.

Uamuzi huu umepokelewa kwa shangwe kubwa na watetezi wa haki za wasichana na watoto kwa kuwa wapo ambao walipata ujauzito kwa kubakwa na siyo kwamba walijiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi wakiwa masomoni.

Tunaipongeza serikali kwa uamuzi huu kwa kuwa sasa unakwenda kuongeza idadi ya wasichana ambao ndoto zao zingekufa, lakini sasa tutakuwa na watu walioelimika watakaolea watoto wao vyema na kutoa mchango kwenye maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Wengi walijikuta wakikatisha ndoto zao na kushindwa kujiendeleza na matokeo yake kuendelea kupunguza idadi ya wasichana wasomi na wanawake wa baadaye ambao watatoa mchango kwa taifa lao.

Wapo wanaosema uamuzi huo utawafanya wanafunzi wanaojihusisha na mapenzi kuwa ni jambo la kawaida, kwa kuwa hakuna adhabu ya kuwafanya wasiendelee na masomo, bali baadaye watarudi na huenda itachochea ongezeko la mimba za utotoni.

Maswali yaliyopo kwa watu ni Je? ndiyo ruksa mabinti wa umri mdogo kushiriki kwenye kujamiiana, na je, itakuwa kwa mimba moja na mtoto mmoja tu au anaweza kufululiza kupata ujauzito, kujifungua baada ya miaka miwili anarudi shule, mwakani anabeba mimba nyingine na nyingine, pia ataruhusiwa kwenda na mwanaye shuleni na kama kuna vituo vya watoto wadogo shuleni.

Kuna umuhimu maswali haya yakajibiwa na serikali ili kurahisisha utekeleza wa waraka huu na kuwafanya wasome na kufikia malengo yao, ili shuleni pasigeuke kuwa mahali pa kuwaumiza tena.

Lakini ni namna watoto hawa hawa watarudi kwenye shule zile zile ambazo wenzao walijua kuwa walipata mimba, lakini hawajui walipata kwa kukubali, kurubuniwa au kubakwa na huenda kutakuwa na unyanyapaa au kuwaumiza kisaikolojia kuwa tayari wameshaondoka kwenye usichama na sasa ni mama.

Waraka umetaka walimu kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi hawa, jambo ambalo ni muhimu kama litatekelezwa kikamilifu, ili kuwajengea ujasiri wa kukubali hali halisi na kurudi kwenye ndoto zao.

Kadhalika, ni muhimu jamii inayowazunguka nayo ikawa na uelewa wa kutosha utakaosaidia wanafunzi hao kusoma kama wengine badala ya kunyooshewa vidole. Tunaamini waraka huu utatekelezwa ipasavyo, pia ni muhimu ukasambazwa kila mahali ili kuwe na uelewa kwa jamii na wazazi ili waruhusu watoto wao kuendelea na masomo.

Habari Kubwa