Bunge letu sasa lisikubali heshima yake kuchafuliwa

24May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bunge letu sasa lisikubali heshima yake kuchafuliwa

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amedokeza jinsi Wabunge wachache wanavyofanya vitendo ambavyo vinautia doa na kuuchafua mhimili wa Bunge, ambao ndicho chombo kikubwa cha maamuzi nchini.

Spika Ndugai alibainisha hayo alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusiana na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli wa kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutokana na kitendo chake cha kuingia bungeni na kujibu maswali ya wabunge yaliyoelekezwa kwa wizara yake aliwa amelewa Ijumaa iliyopita.

Ndugai alifichua kwamba kuna wabunge wachache ambao huingia kwenye ukumbi wa Bunge wakiwa wametumia vilevi vikali zaidi vikiwamo bangi, viroba na dawa za kulevya. Kwa mujibu wa Spika, vikao vya jioni kuwa na waliotumia vilevi wengi zaidi kulinganisha na vikao vya asubuhi.

Hata hivyo, Spika Ndugai alieleza kwamba hivi sasa wanafikiria kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo vinavyovunja heshima ya mhimili huo, ikiwamo kuweka vifaa maalum vya kupima ulevi kwa Wabunge sambamba na kutafuta wataalamu wa ushauri nasaha watakaowapa msaada wa kisaikolojia.

Tunampongeza Spika kwa kufichua kuhusu ukubwa wa tatizo hilo pamoja na hatua ambazo mhimili huo unapanga kuzichukua kwa lengo la kudhibiti vitendo hivyo ambavyo mbali na kuchafua heshima ya Bunge, pia vinakiuka sheria ya kazi na maadili ya jamii yetu.

Sheria ya Ajira na Mahusiano sehemu za kazi ya mwaka 2004 inataka mtumishi kuingia kazini akiwa na akili timamu, hivyo kitendo cha kulewa ni kinyume chake. Kanuni za utumishi wa umma pia haziruhusu vitendo vya aina hiyo kufanywa na mtumishi wa umma.

Pia maadili ya kitaaluma na ya uongozi wa umma yanazuia vitendo kwa watumishi na viongozi wa umma kulewa wakiwa katika sehemu za kazi.

Bunge kama mhimili nalo lina maadili kwa watumishi wake, hivyo wabunge wote wana wajibu wa kuyazingatia ikizingatiwa kuwa mbunge anawakilisha wananchi wengi katika chombo hicho.

Kutokana na Bunge kuwa chombo cha kufanya maamuzi makubwa ya nchi, ikiwamo kutunga na kurekebisha sheria za nchi, Wabunge wanapaswa kujitambua kwa kuzingatia kanuni, sheria na maadili ili kujijengea heshima wao binafsi na Bunge kwa ujumla.

Kadhalika, mbunge kama sehemu ya Baraza la Madiwani la halmashauri yake, bado anatakiwa kuzingatia na kufuata maadili ya baraza husika. Aidha, mbunge anabanwa kuzingatia maaadili ya chama chake kwa kuzingatia kuwa ni sehemu ya viongozi wa chama husika.

Tunaamini kuwa kuheshimu na kufuata sheria, kanuni na maadili ndiyo njia pekee itakayolifanya Bunge letu na mbunge mmoja mmoja kuendeleaa kuheshimika katika jamii yetu. Vinginevyo mhimili huo utapoteza heshima, jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi.

Ni matarajio yetu kwamba hatua alizoahidi Spika Ndugai kuwa zitachukuliwa, na ikibidi kanuni zibadilishwe kwa lengo la kuwadhibiti Wabunge wachache wanaofanywa vitendo vinavyolidhalilisha Bunge zitachukuliwa haraka bila kumlinda au mumuonea mbunge yeyote.

Bila kuchukuliwa hatua hizo, tunakuwa tunalikosesha heshima na hadhi Bunge letu kwa wananchi na kwa mihimili mingine ya Serikali na Mahakama pamoja na kupotosha maana nzima ya dhana ya mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili ya dola.

Habari Kubwa