Changamoto ya TPSF kuhusu kilimo, viwanda ifanyiwe kazi

17Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Changamoto ya TPSF kuhusu kilimo, viwanda ifanyiwe kazi

KATIKA moja ya jitihada za kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda nchini, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),

Imetoa changamoto kwa serikali kulifanya eneo la kuendeleza kilimo katika Ukanda wa Nyanda za Juu (Sagcot) kuwa maalum ukanda wa viwanda kwa mazao ya biashara ili kuchocheo maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, amesema maendeleo ambayo Sagcot imeyapata kuendeleza kilimo katika ukanda huo, ni ya kujivunia na vema serikali nayo ikapeleka nguvu zaidi kwenye viwanda.

Kwa mujibu wa Simbeye, taasisi hiyo inaiomba serikali kwamba katika kutekeleza azma yake ya kuifanya Tanzania nchi ya viwanda itoe kipaumbele kwa ukanda wa Sagcot. Anasema uhamasishaji wa kujenga viwanda utakapofanywa, thamani ya mazao itaongezeka na wakulima watanufaika na kilimo.

Tunakubaliana na ushauri huo kwa kuwa lengo ni kuimarisha kilimo na kuinua uzalishaji wa mazao kwa upande mmoja, lakini pia ni kuhakikisha mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda uliobuniwa na serikali ya Rais John Magufuli unafanikiwa.

Ikumbukwe kwamba kilimo na viwanda ni sekta zinazotegemeana. Viwanda haviwezi kuzalisha bila kilimo ambacho ndicho kinachotoa malighafi za kutumia viwandani. Vile vile, kilimo hakiwezi kuwa na manufaa kama hakuna viwanda kwa kuwa malighafi zinazozalishwa zinahitajika viwandani kutengeneza bidhaa.

Hata mataifa tajiri yenye viwanda yalifikia hatua hiyo kwa kuimarisha kilimo kwanza kisha kufikia mapinduzi ya viwanda kuanzia Uingereza katika karne ya 18 na zingine karne ya 19.

Kipindi hiki ambacho mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda umeshika kasi, kuna maswali ambayo yamekuwa yanakosa majibu, likiwamo je, viwanda vitawezaje kuzalisha bidhaa kama kilimo hakitaimarishwa na kuzalisha malighafi za uhakika kwa ajili ya kutumika viwandani?

Hata hivyo, ushauri wa TPSF umekuja na majibu ya uhakika, hivyo kuna kila sababu kwa wadau na umma kwa ujumla kuunga mkono ushauri huo.

Kwa upande mwingine, serikali hainabudi kuupokea ushauri huo na kuufanyia kazi kisha iamue kulifanya eneo la Sagcot kuwa maalum ukanda wa viwanda kwa mazao ya biashara na maeneo mengine yafuatie.

Ushauri wetu ni kwamba serikali iamue haraka kuhusu hilo kwa kuwa hakuna kitakachopotea kwani mazao yanayohitaji kusindikwa viwanda vitakuwa huko huko.

Tunaipongeza TPSF kwa kuahidi sekta binafsi kuunga mkono jitihada za Sagcot na hasa kuhamasisha kilimo cha biashara na kuinua wakulima wadogo wadogo.

Uhamasishaji wa kilimo cha biashara ni muhimu zaidi kwa kuwa wakulima watazalisha mazao wakijua yatapata soko kutokana na kuhitajika viwandani, tofauti na miaka ya karibuni ambapo walikuwa wanakosa soko na kujikuta vyama vya ushirika vikiyanunua kwa mkopo na kuchukua muda mrefu bila kuwalipa.

Ahadi ya TPSF ya kuwaendeleza wakulima wadogo ni muhimu na ya kupongeza kwa kuwa nchi yetu ina idadi kubwa ya wakulima wadogo ambao ndio tegemeo. Changamoto kubwa na ya muda mrefu ambayo ilikuwa kikwazo kwao ni kukosa uwezo kwa maana ya mitaji kwa ajili ya mbegu, mbolea na dawa za kuulia wadudu.

Hili likifanyika sambamba na kuwapatia mafunzo wakulima wadogo, ni dhahiri uzalishaji wa mazao utaongezeka mara dufu na kuviwezesha viwanda kupata malighafi ya uhakika.

Habari Kubwa