Corona isiwe chanzo wachezaji kula bata

23Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Corona isiwe chanzo wachezaji kula bata

DUNIA kwa sasa imefunikwa na wimbi zito la shambuliio la virusi vya corona (COVID-19), ambavyo havijapata tiba wala kinga na maelfu ya watu wakiendelea kupoteza maisha kila uchao.

Virusi hivyo vilivyoanzia mji wa Wuhan nchini China, tayari vimeenea zaidi ya nchi 188 duniani kote, huku hadi jana ikiripotiwa kuwa zaidi ya watu 13,071 wameshafariki dunia kutokana na virusi vya corona na wagonjwa wakiwa ni zaidi ya 308,720.

Hata hivyo, licha ya kuanzia China, si tishio sana nchini humo kutokana na Wachina kujitahidi kufuata masharti ya namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari zote stahiki zinazoelezwa kuleta matokeo chanya.

Kwa sasa nchi inayosumbuliwa sana na virusi hivyo ni Italia na imeripotiwa zaidi ya 546 wamepoteza maisha ndani ya saa 24 nchini humo hivyo kufanya idadi ya watu waliopoteza maisha hadi jana alasiri kufikia 4,825.

Tayari Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza COVID-19 kuwa janga la kimataifa ('global pandemic'), wakati huu kwa Tanzania kukiripotiwa kuwa na wagonjwa 12 waliopata maambukizi ya virusi hivyo.

Hatua hiyo imesababisha shughuli zote za kijamii, kisiasa, matamasha, michezo na burudani ambazo zinasababisha mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima kupigwa marufuku kwa kipindi cha mwezi mmoja hapa nchini.

Lakini kuanzia shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu vikifungwa kwa kipindi hicho wakati serikali ikifanya tathimini na kuangalia kasi ya maambukizi na namna ya kuzuia kabisa au kutafuta dawa.

Ni wazi, kuzuiwa kwa michezo kuendelea kumeathiri pia Ligi Kuu Bara ambayo ilikuwa ikielekea ukingoni kufuatia baadhi ya timu kuingia raundi ya 29. Hivyo, kwa sasa klabu zote kuanzia ngazi ya chini hadi Ligi Kuu zimetoa mapumziko kwa wachezaji wake kwa muda wote wa zuio hilo la serikali.

Kwa mantiki hiyo licha ya kusimama kwa ligi hiyo, tunaamini wachezaji watakitumia vema kipindi hiki cha mapumziko katika kufanya mazoezi yao binafsi ili kujiweka tayari kuzipambania klabu zao baada ya kipindi hicho kumalizika.

Hatutarajii kuona wachezaji wakikitumia kipindi hiki kufanya starehe ('kula bata') kupindukia hadi kusahau kufanya mazoezi yao binafsi ili kujiweka fiti kwa ajili ya kurejea kumalizia msimu huu wa ligi.

Tunasema hivyo kutokana na kutambua kujisahau kwa wachezaji wanaocheza soka hapa nchini hususan wazawa, ambao wengi wao suala la mazoezi binafsi ni ndoto kwao.

Tunatarajia kuona wakati Ligi Kuu itakaporejea makocha wakianzia pale walipoishia na si kuanza upya kufanya kazi ya ziada ya mazoezi ya kupunguza uzito na kuwajenga wachezaji stamina, kwani matarajio yetu kwao ni kuwaona wakiendelea kujifua wenyewe.

Aidha, kwa kuzingatia hayo, ni wakati pia kwa wachezaji ambao walikuwa wakisugua benchi katika klabu zao kutokana na kushindwa kwenda na kasi ya ushindani wa namba, wakitumia mapumziko haya ya dharura kujiimarisha binafsi.

Mashabiki na wadau wa soka matarajio yao kama ilivyo kwa Nipashe, ni kuona ubora na ushindani ukiongezeka pindi ligi itakaporejea na si kuanza kwa kujisuasua kama mwanzo wa msimu.

Hivyo, wachezaji hawana budi kulitambua hilo na kulifanyia kazi badala ya kuona kwamba wamefunguliwa milango ya kwenda kula bata uraiani.

Habari Kubwa