Dar chukueni hatua UVIKO-19 bado ipo

10Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dar chukueni hatua UVIKO-19 bado ipo

TAARIFA iliyotolewa juzi na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichwale, inaonyeha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watu waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa UVIKO-19.

Kwamba, mkoa huo una wagonjwa wapya 184 kati ya visa vipya 252 vilivyoripotiwa, ambavyo vimeripotiwa katika kipindi cha Januari 29 hadi Februari 6, mwaka huu, huku wagonjwa wapya 76 kati ya 78 waliolazwa wakiwa ni ambao hawajachanjwa na vifo vilikuwa vitatu.

Mganga huyo anafafanua kuwa tangu ugonjwa huo ulivyoripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Machi 2020 hadi kufikia Februari 6, mwaka huu, jumla ya watu 33,482 walithibitika kuugua sawa na asilimia 7.6 kati ya 442,566 waliopima na jumla ya watu 792 wamepoteza maisha.

Kutokana na takwimu hizo, Wizara ya Afya inawataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo, ikiwamo kuchanja chanjo ya UVIKO-19.

Lakini pia anasema serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo nchini, ili kuwezesha wananchi kupata kinga ya ugonjwa huo, na kwamba hadi Februari 6, mwaka huu, dozi 9,845,774 za chanjo zilikuwa zimepokewa nchini.

Kwa mujibu wa Mganga huyo Mkuu, tangu kuanza kwa zoezi la uchanjaji nchini mpaka kufikia Februari 6, mwaka huu jumla ya watu 2,117,387, sawa na asilimia 3.67 wamepata dozi kamili ya chanjo.

Pamoja na hayo, anawataka wananchi kuhakikisha wanapata dozi kamili za chanjo, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa kwa usahihi, kuzingatia usafi binafsi kwa kunawa mikono, kuwahi kwenye vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa huo na kuzingatia kufanya mazoezi.

Kimsingi, taarifa hiyo imeweka wazi ukweli halisi kuhusu ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo nchini kwa takwimu za Mkoa wa Dar es Salaam, ambao unachukuliwa kuwa na idadi kubwa ya watu.

Kutokana na hali hiyo, nasi tunadhani kwamba si wakati wa kuendelea kupuuza kuhusu uwapo wa ugonjwa huo na athari zake, hivyo wakazi wa Dar waache kulala bali kila mmoja achukue tahadhari zote zinazotakiwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo, kwani ni wazi kwamba wakazi wengi hawafuati maelekezo.

Mitaani mikusanyiko inaendelea kama kawaida, ndani ya usafiri wa umma hasa daladala abiria wanajazana kama kawaida, karibu wote hawavai barakoa kana kwamba ugonjwa huo haupo nchini.

Katika mazingira hayo, tunaona kuna haja ya kuwakumbusha wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzingatia maelekezo yote yanayohusu kujikinga na ugonjwa huo hatari ikiwamo kujitokeza kupata chanjo yake inayotolewa bure.

Ikumbukwe, Mganga Mkuu anasema, visa vimeripotiwa katika kipindi cha Januari 29 hadi Februari 6, mwaka huu, huku wagonjwa wapya 76 kati ya 78 waliolazwa wakiwa ni wale ambao hawajachanjwa na vifo vikiwa ni vitatu.

Hapo tushauri kwamba, hali hiyo inatosha kuamsha wananchi kuwa makini kwa kuchukua tahadhari zote, ikiwamo kujitokeza kwa wingi kwenda katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kutolea chanjo ya UVIKO-19.

Takwimu hizi zinapaswa kuwazindua Watanzania kwamba kupata chanjo ya UVIKO-19 ndiyo njia sahihi na salama kwa maisha yao kwa kuwa zimethibitisha kuwa wanaokaidi kuchanja ndio wanaokufa na kupata maambukizi.

Tunaona mkazo unaosisitizwa, ni wananchi wajitokeze kupata dozi kamili za chanjo, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa kwa usahihi, kuzingatia usafi binafsi kwa kunawa mikono, kuwahi kwenye vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa huo na kuzingatia kufanya mazoezi.

Tangu mwishoni mwa Julai mwaka jana, chanjo ilipozinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan, inaelezwa kuwa ni watu 2,117,387, sawa na asilimia 3.67 ambao wamepata dozi kamili ya chanjo. Kwa takwimu hizi ni wazi kuna kusuasua katika kujitokeza kupata chanjo, na ikumbukwe kuwa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla siyo kisiwa kisichofikika, hivyo wananchi wajitokeze kuchanja.

Habari Kubwa