Dar inahitaji mpango kuyaondoa mafuriko

15Oct 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dar inahitaji mpango kuyaondoa mafuriko

JUZI mvua kubwa ilinyesha jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya saa 12, na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi, uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu na vifo vya watu wanane wakiwamo watoto wawili.

Kutokana na mvua ya siku moja barabara zote za lami na changarawe zilikuwa taabani kutokana na miundombinu kushindwa kuhimili maji ya mvua, kwa mitaro kujaa maji mengi kiasi cha kushindwa kuonekana kingo zake.
 
Barabara zote za kuingia na kutoka ndani ya jiji zilizidiwa na maji kiasi cha vyombo vya usafiri kama magari yaliingia maji ndani, kuharibika, kingo za madaraja kubomoka, makalavati kuzolewa na maji huku kuta za nyumba zikibomoka na kuta nyingine za fensi za nyumba.
 
Pia taarifa zinaeleza watu kadhaa walijeruhiwa, na wengine walifika nyumbani usiku wa manane na wengine kuamua kulala sehemu tofauti na nyumbani ili kubaki salama.
 
Kwa ujumla, mvua hiyo ilionyesha uhalisia wa miundominu ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia barabara za ndani na nje katika kubeba maji mengi ya mvua kwa wakati mmoja.
 
Picha za video zilionyesha magari yalivyokwama, yalivyoingia maji ndani na madereva kutumia vikopo kuchota, baadhi ya nyumba eneo la Jagwani zilifunikwa kabisa na kwingine hakupitiki.
 
Katika barabara ya Mwenge Morocco ambako ujenzi unaendelea hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kuwa miundombinu hiyo mipya hakuweza kumudu maji ya mvua, jambo ambalo linaonyesha bado kuna jambo linatakiwa kufanyika kabla ya kukabidhiwa kwa barabara hiyo.
 
Kwa barabara za ndani ya makazi ya watu ambazo nyingi ni za kiwango cha changarawe zilikuwa taabani kiasi cha kushindwa kupitika, huku magari yakikwama na kuharibika kwenye maeneo ya mabonde.
 
Maeneo ya Posta, Muhimbili, Upanga na Mikocheni, Masaki nako hali ilikuwa hivyo hivyo wenye magari walionekana wakitaabika kupita huku magari yakizidiwa na maji na baadhi ya shule maji yakiingia madarasani kiasi cha masomo kuahirishwa.
 
Eneo la Tegeta na Bunju nyumba nyingi ziliingiliwa na maji, hali inayodhihirisha kuwa miundombinu ya jiji bado inahitaji matengenezo makubwa ili wananchi waishi kwa amani majira yote ya mwaka.
 
Imekuwa kawaida kila kunapokuwa na mvua lazima majanga yatokee, ikiwamo barabara kujaa maji kwa kuwa miundombinu iliyopo haiwezi kumudu maji ya mvua.
 
Hili ni fundisho kwa makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara kujua kuwa inahitajika miundombinu inayoweza kumudu maji ya mvua nyakati zote na kuyapeleka baharini.
 
Pia, wapo wananchi waliojenga maeneo yasiyotakiwa kwa maana ni bondeni, kando mwa mito na mkondo wa maji, lakini bado hawaondoki licha ya usumbufu wanaokutana nao kila majira ya mvua.
 
Mvua hii ni ya siku moja na itaendelea zaidi kwa kuwa sasa tunaelekea kwenye miezi ya mvua kila siku, maana yake kila mwananchi achukue tahadhari kuhakikisha wanakuwa salama.
 
Kwa wajenzi wa miundombinu wahakikishe inajengwa inayomudu maji ya mvua nyakati zote na si  nyakati za ukame pekee, kila nyakati za mvua hali halisi huonekana, lakini bado hali imekuwa ile ile.
 
Ilitarajiwa ujenzi unaofanyika sasa kuendana na hali halisi ya maji ya mvua hasa yanapokuwa mengi, lakini hali ni tofauti.
 
Pia mvua hizi zinatufundisha kuwa miundombinu ya kwenye makazi ya watu bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kwamba inatakiwa kujengwa ili wananchi waweze kupita kutoka eneo moja kwenda jingine.

Hili tatizo linaweza kuisha kabisa ikiwa kunakuwapo na mpango mkakati wa kuliboresha Jiji la Dar es Salaam; kubwa zaidi ni kutengwa fedha katika bajeti za kila mwaka kwa ajili ya kujenga mfumo imara wa mifereji ya kuelekeza maji yanapotakiwa kwenda (baharini).

Kadhalika, sheria zilizopo zitumike kuwadhibiti wale wote wanaojenga kiholela bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ujenzi.

Habari Kubwa