Diaspora, mabalozi wamuige Rais Magufuli

31May 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Diaspora, mabalozi wamuige Rais Magufuli

RAIS John Magufuli, ametangaza habari njema kwa wakulima wa mahindi ambao wamepata soko la kuuza nafaka hiyo, nchini Zimbabwe, ambayo kuanzia sasa itanunua tani 700,000 za zao hilo kutoka nchini.

Jitihada hizo za Rais ni wazi zitawanufaisha wakulima wengi ambao walikuwa na kilio cha kukosa soko la kuuzia mahindi yao, ambayo yalikuwa hayana mnunuzi katika soko la ndani.

Alichofanya Rais pamoja na kudumisha ushirikiano wa nchi za Afrika Kusini kinaongeza pia hamasa kwa wakulima wa mahindi ambao wamepata fursa ya kuzalisha na kuwekeza zaidi kwani kuna uhakika wa soko.

Ni wazi kuwa pamoja na Zimbabwe mataifa kama Kenya, Ethiopia, Uganda, Malawi, Msumbiji na Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na mafuriko ambayo huenda yakasababisha njaa na kuhitaji chakula kutoka Tanzania.

Tunaona kuwa hii nayo ni fursa ya kuuza mazao yanayozalishwa kwa wingi nchini ukiwamo muhogo, maharage na jamii nyingine za nafaka.

Tukizungumzia mihogo ni zao ambalo limezalishwa kwa wingi kwa miaka ya hivi karibuni, lakini halijapata soko la uhakika hasa kutokana na ukosefu wa viwanda vya kutosha vya kusindika na kuchakata bidhaa nyingine zinazotokana na mihogo.

Ni wazi kuwa kama walivyo wakulima wa mahindi, wanaozalisha mihogo nao wangependa juhudi zao kupata fursa ya kuwezeshwa kuuza nje ya mipaka.

Kwa hiyo tunaona ni vyema mabalozi na wana diaspora walioko katika nchi mbalimbali kusaidia juhudi za wakulima kupata masoko ya mazao ya chakula yanayozalishwa kwa wingi kama ambavyo Rais amefanya kwa muda mfupi alipoitembelea Zimbabwe.

Ni wazi kuwa mataifa mengi ya Afrika yanatumia unga wa mahindi au muhogo kama chakula kikuu na Tanzania ni moja ya mataifa wazalishaji wakubwa wa muhogo na mahindi.

Kwa wakulima hii ni fursa kuzalisha unga ulioongezewa thamani ukiwamo wa muhogo na mahindi ambao unaweza kuuzwa kwenye mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Afrika ambayo yamekumbwa na mafuriko, ukame na njaa.

Ni jukumu la wawakilishi wakiwamo mabalozi na wana diaspora kutafuta masoko hayo, ili kukuza uzalishaji na uchumi wa raia taifa hili.

Aidha, mazao kama maharage huzalishwa kwa wingi nchini na ni chakula kinachotumiwa na nchi nyingi duniani kuanzia Afrika, Asia, Uarabuni na Uchina.

Tanzania imebarikiwa kuwa na aina mbalimbali tena bora za maharage yakiwamo soya inayozalishwa Mbeya.

Tunaona ni wakati wa kusaka masoko ya mazao hayo na kuwanufaisha wakulima wetu. Japo zama hizi kinachosisitizwa ni kujenga viwanda ili kuyaongezea thamani, vyote hivyo vinaweza kufanyika ili kukuza uchumi wa taifa na kuongeza wigo wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Chakula ni mojawapo ya mahitaji makubwa barani Afrika mathalani uwapo wa soko kubwa linalopatikana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hata Sudan Kusini.

Tunashauri kufunguliwa magulio na masoko ya nafaka hasa mahindi, mtama na muhogo ambayo yatawaalika wafanyabiashara kutoka nchi hizo na nyinginezo kuja kununua mazao hayo hapa nyumbani.

Kama yalivyo magulio na masoko ya dhahabu ni vyema pia kuwa na magulio ya mazao ya chakula ili kuwapa nafasi wafanyabiashara wa nje kuja nchini kununua bidhaa hizo.

Habari Kubwa