Dirisha dogo la usajili liwe la kujenga si kukomoana

15Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dirisha dogo la usajili liwe la kujenga si kukomoana

USAJILI wa dirisha dogo kwa ajili ya wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza), First League (Ligi Daraja la Pili) na Ligi Kuu ya Wanawake nchini linatarajiwa kufungwa leo saa 5:59 usiku.

Lengo la dirisha hili dogo la usajili ni klabu kupata nafasi ya kurekebisha na kuimarisha vikosi vyake kutokana na mapungufu waliyoyabaini katika mechi ambazo wameshacheza katika ligi husika wanazoshiriki, mashindano ya kimataifa na michuano ya Kombe la FA.

Klabu itakayotumia vyema dirisha hili dogo la usajili, hakika matunda yake yataonekana ndani ya muda mfupi na si vinginevyo.

Timu zitakazowaachia makocha wao kufanya mchakato wa safu ipi inahitaji kuboresha, hakika itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo chanya baada ya kusajili wachezaji wapya katika dirisha hili lililofunguliwa tangu Desemba 15, mwaka jana.

Kama ambavyo timu husika inafahamu mahitaji yake halisi, na ikayatendea haki, ni ukweli usiofichika timu hiyo itarejea katika hatua ya mwisho ya lala salama ya msimu ikiwa imara na ikielekea kwenye kutimiza ndoto na malengo yake iliyojiwekea katika msimu huu wa mwaka 2021/22.

Timu inaweza ikakumbana na changamoto ya fedha katika kukamilisha usajili wake, lakini bado inatakiwa kuwa na suluhisho au machaguo yanayozidi mawili ili kufanikisha lile ambalo inalihitaji kwa ajili ya kuboresha kikosi chake ambacho kiko kwenye mbio za ubingwa au kujinusuru na kushuka daraja.

Lakini katika hali isiyo ya kawaida, kuna klabu zinaendelea na mchakato huu bila kuhusisha makocha wake ambao kwa taaluma yao wanajua mahitaji halisi ya timu yao na wanachohitaji ili kufikia malengo ya kucheza soka la ushindani wakati wote.

Itashangaza kuona katika dunia ya sasa bado viongozi wa timu za hapa nchini wanasajili wachezaji wapya kwa shinikizo kutoka upande fulani au kumkomoa mpinzani wako. Ieleweke kufanya hivyo si tu kuiumiza timu yao, lakini pia ni kukiweka mashakani kipaji cha mchezaji husika.

Kusajili mchezaji ambaye hayuko katika mipango ya kocha ni jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya timu au ligi kwa ujumla, lakini pia inapoteza nafasi ya mchezaji kuendeleza kipaji chake. Ili kuachana na 'mauzauza' haya, umefika wakati makocha wakapewa nguvu na viongozi wakabakia na nafasi yao ya kukamilisha taratibu za kiutawala.

Mpaka sasa kwenye ligi zote zinazochezwa hapa nchini hakuna timu ambayo iko salama katika mbio za ubingwa au kwa wale wanaoburuza mkia kusema ni lazima watashuka daraja. Muda wa kufanya marekebisho kwa weledi bado upo na saa chache zilizobakia zinaweza kubadilisha mwelekeo wa timu husika.

Kikubwa ili kufikia malengo, viongozi wanatakiwa kuwapa makocha nafasi ya kukamilisha mchakato huu kikamilifu na hapo baadaye timu itakapofanya vibaya, watawajibika kutoa maelezo huku hatua nyingine zinaweza kuchukuliwa kulingana na makubaliano wakati wanakabidhiwa mikoba ya kufundisha timu hizo.

Tunawakumbusha ligi zote bado ni changa na mpaka sasa hakuna klabu ambayo iko salama kwenye kufikisha malengo yake ndani ya msimu huu. Lolote linaweza kutokea na kubadilisha msimamo uliopo sasa na kuwashangaza wote ambao waliamini msimu huu kwao unaweza kuwa wa furaha.

Ni jambo la kushangaza baadhi ya timu zinaanza kurudi kule ambako tulishakusahau kwa kugombea mchezaji ambaye kwa 'macho' ya nje tayari alishafanya mazungumzo na timu nyingine, hili linaweza kuwa na faida endapo nyota huyo atafanya vyema, lakini itaonekana 'mkosi' endapo mchezaji huyo husika atashindwa kuonyesha kiwango bora baada ya kusajiliwa.

Jambo la msingi na la kuzingatiwa kwa maendeleo ya soka hapa nchini kwenda kwa wahusika wote ni kufahamu dirisha dogo la usajili linatakiwa kutumiwa kwa maana halisi iliyowekwa na kamwe isiwe kwa 'kukomoana' kwa sababu kwa kufanya hivyo, klabu husika haitafaidika lakini pia nafasi ya kuendeleza timu au maslahi ya mchezaji huenda yakawa shakani.

Kwa maendeleo ya timu, ni vyema kutumia saa chache zilizobakia kabla ya dirisha la usajili halijafungwa, kukamilisha michakato itakayojenga na si vinginevyo maana hakuna mechi rahisi msimu huu.

Habari Kubwa