Dk. Mengi ametuachia mazuri mengi, yaenziwe

03May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dk. Mengi ametuachia mazuri mengi, yaenziwe

MWENYEKITI Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi Dubai, Falme za Kiarabu.

Dk. Mengi ambaye alizaliwa Mei 29, 1942, ni mmoja wa mabilionea barani Afrika, alipatwa na umauti usiku wa kuamkia jana, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na familia yake na kutolewa na vyombo vya habari vya runinga na redio vya IPP.

Taasisi za kitaifa na kimataifa na makundi mbalimbali ya kijamii yalionyesha kuguswa na msiba huo na kutuma salamu za rambirambi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Ni dhahiri kuwa jamii imeguswa sana na msiba huo mzito na pengine ndio maana wengi wameelezea kusikitika, akiwamo Rais John Magufuli ambaye alisema alieleza kusikitishwa na kwamba  atamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa na maono yake yaliyopo katika kitabu cha 'I Can, I Must, I Will'.

Hatutaweza kueleza kwa undani kila mmoja amesema nini, lakini itoshe tu kueleza kuwa Dk. Mengi alikubalika sana katika jamii kutokana na kujitoa kwake kusaidia watu wengi waliohitaji msaada pamoja na ushauri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha.

Katika baadhi ya mambo ambayo mchango wake hautasahaulika ni kujitoa kwake kusaidia watu wenye ulemavu. Kwa takribani zaidi ya miaka 20 amekuwa akiwasaidia watu hao kwa njia mbalimbali ikiwamo kukaa na kula nao chakula kila mwaka, akieleza kuwa anafanya hivyo kwa kuwatambua wa kundi hilo kuwa ni sawa na binadamu wengine.

Kutokana na kuguswa na kuthamini mchango wake huo, serikali ilimshauri kuanzisha taasisi ya watu wenye ulemavu ili na serikali iangalie uwezekano wa kupitisha msaada wa kulisaidia kundi hilo.

Ushauri huo aliuzingatia kwa kuanzisha taasisi hiyo, ambayo aliitumia mwaka jana kutoa tuzo kwa watu wenye ulemavu waliofanya vizuri katika mambo mbalimbali katika jamii.

Pia Dk. Mengi atakumbukwa na jumuiya ya wafanyabiashara ndani na nje, kutokana na mchango wake alioutoa ikiwamo kuongoza taasisi mbalimbali za wafanyabiashara. Miongoni mwa hizo ni Baraza la Taifa ka Biashara (TNBC), Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara Afrika Mashariki na

mkurugenzi katika jumuiya ya wafanyabiashara wa Jumuiya ya Madola, kwa kutaja baadhi.

Kadhalika, Dk. Mengi katika uhai wake alisimamia na kusaidia miradi kadhaa ikiwamo ya kulinda na kuhifadhi mazingira pamoja na ya kupambana na umaskini, ikiwamo kuanzisha vikundi vya kusaidia vijana kupambana na umaskini.

Vile vile, atakumbukwa na wanataaluma wa tasnia ya habari kutokana na uwekezaji mkubwa, ambao uliwezesha wengi kupata ajira pamoja na kutetea haki za waandishi wa habari. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Dk. Mengi ameacha alama katika jamii, tukimaanisha kuwa ameacha mazuri mengi ambayo tunapaswa kuyaendeleza kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Kitabu chake cha 'I Can, I Must, I Will' ni urithi kwa wengi ambao wana kiu ya kuondokana na umaskini na kupata mafanikio katika maisha, hivyo ni muhimu Watanzania tukakisoma na kuzingatia aliyoyaeleza kuhusiana na siri ya kufanikiwa.

Hakika alikuwa mtu wa kuthubutu. Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi. Amen.

Habari Kubwa