Dozi za corona zinaendelea kuletwa, twende kuchanja

25Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dozi za corona zinaendelea kuletwa, twende kuchanja

TANZANIA imeendeleza juhudi za kupambana na tishio la corona, baada ya juzi serikali kupokea chanjo 499,590 za aina ya Pfizer-Biontech kupitia mpango wa COVAX Facility kutoka Marekani ambazo zitakinga Watanzania 249,795 watakaopatiwa dozi hiyo mara mbili.

Lakini tangu kampeni ya chanjo ya ugonjwa huo izinduliwe na Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa Julai mwaka huu, nchi imeshapokea jumla ya dozi 1,227,400 za Jensen ambazo zinakinga Watanzania 1,227,400.

Vilevile, dozi 2,578,400 za Sinopharm ambazo zinakinga Watanzania 1,289,200, na juzi zimepokelewa dozi 499,590 za Pfizer, huku Watanzania 1,359,624 wakiwa tayari wamechanjwa.

Tangu kampeni ya chanjo kuzinduliwa, sasa ni karibu miezi minne imepita, na idadi ya waliochanjwa inendelea kuongezeka kutokana na hamasa na elimu kwa umma.

Hapa ttunaona ipo haja ya kuongeza kasi ya uhamasishaji ili watu wajitokeze wengi zaidi kuchanjwa. Ni muhimu jamii ikahamasishwa na kujitokeza kwa wingi, kuchanjwa kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza mlipuko wa ugonjwa huo ambao unaelezwa kuwa umeanza kuibuka upya katika nchi za wenzetu.

Tunahimiza umuhimu wa kuchanjwa kutokana na ukweli kwamba, Tanzania siyo kisiwa, bali ni nchi kama nyingine, na inaweza kukumbwa na na ugonjwa huo wakati wowote, hivyo tunashauri uhamasishaji na elimu ya chanjo upewe mkazo.

Mikoa 10 ikiwamo ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Dodoma, Arusha, Mwanza, Ruvuma, Mbeya, Morogoro, Mtwara na Kagera, inatajwa kuwa vinara wa kuchanja watu wengi zaidi.

Ingekuwa ni nafasi nzuri kwa viongozi wa mikoa mingine kujifunza kutoka katika mikoa hiyo, jinsi ambavyo imefanikiwa kuchanja watu wengi ili nao nao wapeleke mbinu hizo mikoani mwao.

Ingawa suala la chanjo ni hiari, lakini kwa kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa, tunaona kuwa ipo haja kwa serikali kufika mahali ikapima utendaji wa viongozi wake ngazi za mikoa na wilaya kwa kutumia kigezo cha ufanisi wa chanjo ya corona.

Njia hiyo pia tunadhani inaweza kuongeza kasi ya watu kuachana na elimu ya mitaani inayopingana na chanjo, badala yake watu wanaweza kujitokeza kwa wingi kulinda afya zao dhidi ya ugonjwa huo.

Viongozi na watendaji wa ngazi zote wanaelekezwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha wananchi wanahimizwa kwenda vituo vya kutolea huduma hiyo kwa kuwa vita hii ni ya watu wote.

Hivyo wawe ni viongozi wa dini, siasa, asasi za kiraia, tunaona ni vyema washirikiane na serikali katika kuelimisha na kuhamasisha umma wa Watanzania kuona umuhimu wa kuchanjwa.

Kumekuwapo na taarifa kuwa baadhi ya wanaume huwazuia wake zao kwenda vituoni kupata chanjo, kama watu wa aina hiyo wapo, basi tunashauri mamkala husika kufuatilia na kuchukua hatua kwa wahusika.

Tunashauri hivyo, kwa sababu afya ni jambo nyeti, ni vyema mtu akaachwa awe huru kuchanja au kutochanja au aelimishwe aelewe kisha achukue hatua, badala ya kuzuiwa kama ambavyo imewahi kuripotiwa.

Jambo ambalo ni muhimu kuzingatia katika kukabiliana na ugonjwa huo, ni kwamba Tanzania siyo kisiwa hadi isifikiwe na ugonjwa huo, bali ni vyema kuchukua tahadhari kwa kuchanjwa.

Katika Kiswahili, kuna msemo kwamba; 'Kinga ni bora kuliko tiba', hiyo tunashauri umuhimu wa kuzingatia kinga kwa kujitokeza kwa wingi kuchanjwa badala ya kusubiri kupatwa na UVIKO-19.

Habari Kubwa