Droo nusu fainali FA ifanyike kwa uwazi

20Mar 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Droo nusu fainali FA ifanyike kwa uwazi

HATUA ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania [TFF], maarufu kama Kombe la FA, iliendelea jana kwa Simba kuvaana na Madini FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kadhalika, juzi wapenda soka nchini walishuhudia Mbao FC ikiwa timu ya kwanza kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuitoa Kagera Sugar baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mechi zilizobakia za robo fainali kabla ya droo ya hatua ya nusu fainali kufanyika ni kati ya Yanga dhidi ya Tanzania Prisons na Azam FC dhidi ya Ndanda FC.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo ya msimu huu ambayo Yanga ni bingwa mtetezi, droo imekuwa ikipangwa kwa siri jambo ambalo limezua maswali mengi kwa wadau wa soka, na wengi wakidai kuwa TFF ina lengo la kuzibeba timu za Simba, Yanga na Azam FC ili mojawapo iibuke bingwa kwa kile wanachodai kuwa shirikisho hilo linaamini ndizo zenye uwezo mkubwa wa kuiwakilisha vema nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo, ndiye atakayeiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hapo mwakani.

Michuano ambayo ni ya pili kwa utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga ilitolewa na Zanaco juzi kufuatia faida ya bao la ugenini baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa na kisha suluhu kwenye mechi ya marudiano Zambia.

Kutokana na uwazi na utandawazi kutawala dunia ya leo na hata katika tasnia ya soka, mashabiki, wadau na hata viongozi wa klabu husika katika mashindano hayo wanahaki ya kutaka kufanyika droo ya wazi ili kuondoa hofu hiyo.

Nipashe tunaunga mkono hoja hiyo, ambayo imekuwa mjadala mzito kupitia mitandao ya kijamii sambamba na baadhi ya vyombo vya habari.

Sisi kama wadau wakubwa wa soka, hatuoni sababu yoyote kwa droo hiyo kufanyika kwa kificho wakati tumekuwa tukishuhudia ile ya Caf, Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League ikifanyika kwa uwazi kabisa kupitia runinga.

Siyo hiyo tu, kadhalika michuano ya Kombe la Ligi na Kombe la FA England, droo imekuwa ikifanyika kwa uwazi na hakuna malalamiko yoyote kutokea kwa timu fulani kubebwa zaidi ya kusikia kauli kama "hatukuwa na bahati na droo ama ratiba".

Kwa mantiki hiyo, kuelekea droo ya nusu fainali, Nipashe tunaishauri TFF ifanyike kwa uwazi huku ikishirikisha wajumbe ama kiongozi mmoja mmoja kutoka katika kila klabu zilizotinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Ni wazi tangu awali TFF haina budi kukiri kuwa haikuzitendea haki klabu shiriki katika michuano hiyo kutokana na kutofanyika droo ya wazi ambayo ingekufuta dhana hiyo ya kuwapo kwa baadhi ya timu kubebwa.

Kama lengo la TFF ni kuona anapatikana bingwa wa haki katika michuano hiyo, basi haina budi kufanya droo hadharani na endapo lengo lao ni kuziona Simba, Yanga ama Azam FC mojawapo ikiibuka bingwa na kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, basi michuano hiyo haina maana kwani mshindi wa pili wa Ligi Kuu angeendelea kuwa ndiye anayeiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunasema hivyo kwa kuwa mara nyingi timu hizo ndizo huwa zinamaliza ligi zikiwa nafasi tatu za juu. Chonde chonde TFF, droo ya FA kuanzia sasa ichezeshwe kwa uwazi.

Habari Kubwa