Dua kwa Simba, Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika

16Mar 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Dua kwa Simba, Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika

NI siku nyingine kwa wadau wa soka Tanzania na Afrika Mashariki na Kati wakisubiri kuona wawakilishi wao, Simba wakifanya vizuri katika mechi yao ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo wanatarajia kuwakaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Marefa wa mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 1:00 usiku wanatoka Morocco.

Wekundu wa Msimbazi kama ambavyo hujulikana, wanahitaji matokeo ya ushindi tu ili wajihakikishie tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika.

Nipashe linawatakia mafanikio wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Simba kwa sababu inaamini kusonga mbele kwa timu hiyo kutaendelea kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika medani za kimataifa.

Kwa hatua ambayo Simba imefika, ni vema Watanzania wakaungana kuishangilia na kumaliza kilio cha timu za hapa nchini kuwa wasindikizaji kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa na hatimaye kufungua ukurasa mpya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, aliwaambia Simba wanatakiwa kujituma na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na kusahau kutwaa makombe madogo madogo.

Rais Magufuli aliwaambia Simba anataka kuona wanatwaa ubingwa wa Afrika, na endapo timu hiyo itaibuka na ushindi katika mchezo wa leo, itakuwa inaendelea na safari ya kuwania taji hilo la juu kwa ngazi ya klabu barani hapa na kumfurahisha kiongozi huyo mkuu wa Tanzania.

Gazeti hili linaamini Simba ina nafasi nzuri ya kuandika historia nyingine kwa nchi ambayo pia wiki ijayo itakuwa na jukumu lingine la kupeperusha bendera ya Tanzania katika kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Afrika (AFCON).

Endapo Simba itasonga mbele, itaongeza morali kwa kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa kuamini hakuna kisichowezekana kwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu na si vinginevyo.

Kila mchezaji wa Simba anatakiwa afahamu kuwa michuano hiyo ni fursa nyingine kwao kutangaza vipaji vyao na hivyo wapambane kwa ajili ya klabu yao, taifa na wao binafsi.

Kama Simba itashinda mechi ya leo na kutinga hatua ya robo fainali ambayo mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni mwaka 2003, itawafanya mawakala kutoka nchi mbalimbali kuwafuatilia wachezaji na wale watakaokuwa na bahati watanunulia na kwenda kucheza soka la kulipwa ughaibuni.

Pamoja na utani wa jadi uliopo, ni vema mashabiki wa soka nchini wakaungana kuishangilia Simba katika mechi ya leo ya kwa sababu kufanya vizuri kutasaidia nchi kuwa na nafasi zaidi ya moja katika michuano hiyo mwakani kama yalivyo mataifa mengine.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huu wa kimataifa, utani, ushindani na majigambo yarejee pale watakapokuwa katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya Kombe la FA, ambayo nayo hutoa mwakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa.

Lazima tukubali kuwa safari hii ni zamu ya Simba, hivyo ni vema wakaungwa mkono na utaratibu huu utaendelea kwa kuunganisha nguvu kwa klabu nyingine itakapokuwa inapeperusha bendera ya nchi.
Mungu ibariki Simba SC, Mungu ibariki Tanzania.

Habari Kubwa