Elimu kuhusu sensa kwa umma muhimu

19Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Elimu kuhusu sensa kwa umma muhimu

SENSA ya watu na makazi ni suala muhimu sana kwa kila taifa. Kutokana na umuhimu huo, ndio maana ni takwa la kisera na kisheria.

Umuhimu wa sensa unatokana na kutoa takwimu halisi za idadi ya watu katika nchi, hivyo kuisaidia serikali katika kupanga mipango yake ya maendeleo, ukihusisha huduma za jamii.

Kwa maneno mengine, wataalamu wa mipango wanapokuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu, unakuwa rahisi kwao kupanga mipango ambayo inawalenga watu wote, zikiwamo huduma.

Kwa mfano, serikali haiwezi kuandaa bajeti kwa kutenga fedha za ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya, maji, barabara, madaraja na huduma nyingine muhimu bila kuwa na takwimu halisi zinazohusu idadi ya watu pamoja na makazi.

Hata hivyo, katika nchi yetu baadhi ya wananchi wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu sensa na matokeo yake kuwa wagumu kujitokeza kuhesabiwa, hivyo kukwaza malengo ya sensa.

Kuna wakati baadhi ya jamii zimekuwa zikitoa masharti kwa serikali iyatekeleze ili zikubali kuhesabiwa, ikiwamo kudai kupewa vyakula bila kujua kuwa kufanya hivyo ni kukwaza zoezi hilo lenye lengo zuri la kuwapatia huduma stahiki katika maendeleo kwa ujumla.

Lakini kwa mtazamo wetu tunaona kuwa hali hiyo inasababishwa na kukosekana kwa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Kwa kuona tatizo hili pengine ndio maana Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameitaka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ili kuondokana na imani potofu kwa baadhi ya makabila yanayokataa kuhesabiwa, ikiwamo kuogopa kufa.

Ndugai aliyasema hayo jana jijini hapa kwenye kikao cha uhamasishaji wa utoaji elimu ya sensa hiyo inayotarajiwa kufanyika nchini Agosti, mwakani.

Alisema elimu isipotolewa ipasavyo, itasababisha kukwamisha sensa hiyo kwa kuwa kuna baadhi ya makabila mila zake zinakataa kuhesabu watu wake au mifugo yao.

Alisema kuhesabiwa ni jambo muhimu sana, na kwamba kuhesabiwa si jambo rahisi kwa sababu zipo baadhi ya nchi hazina sensa kwa sababu haziamini katika kuhesabiwa, ingawa jambo la kushukuru ni kuwa Watanzania tumeendelea na zoezi hilo kwa miaka mingi.

Alisema elimu ikitolewa itaondoa mawazo na imani potofu iliyopo kwa baadhi ya makabila nchini yanayokataa kuhesabiwa.

Spika mstaafu, Anne Makinda, ambaye ni Kamishna wa Sensa nchini, alisema kuna umuhimu Tanzania kupata idadi ya watu wake katika kupanga maendeleo ya watu wake na kukuza uchumi.

Kwa kuwa nchi yetu imebaki na takribani mwaka mmoja kabla ya sensa hiyo kufanyika, sisi tunazishauri mamlaka husika za serikali kutoa kipaumbele kwa elimu ya umma, kwa lengo la kuwawezesha wananchi wengi kujua manufaa ya kuhesabiwa.

Ofisi Kuu ya Takwimu (NBS) hainabudi kuweka mipango na mikakati ya kutoa elimu hiyo sambamba na kufanya uhamasishaji kupitia viongozi wa dini, siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari. Tunaamini kuwa hilo likifanyika mapema, bila shaka wananchi wengi watakuwa na uelewa na mwitikio wa kuhesabiwa utakuwa mkubwa.

Habari Kubwa