Elimu kwa mpigakura redio za kijamii itasaidia

10May 2017
Mhariri
Nipashe
Elimu kwa mpigakura redio za kijamii itasaidia

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpigakura kupitia redio za kijamii ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.

Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani, alitoa wito huo wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpigakura nchi nzima ulioanza kutekelezwa Mei 8, mwaka huu katika mikoa 10 nchini.

Alisema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpigakura na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.

Kailima alisema kupitia mpango huo, Tume itasambaa nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpigakura kwenye redio za kijamii zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alitoa wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo Tume itakwenda kutoa elimu ya mpigakura, wasikilize na kuuliza maswali ili waweze kuelewa.

Tunaipongeza NEC kwa kubuni na kuanza kutekeleza mpango huo, ambao tunaamini kuwa utawapa fursa wananchi kuelewa kwa kina mambo mbalimbali yakiwamo haki na wajibu wa mpigakura wakati wa uchaguzi.

Huko nyuma miongoni mwa mambo yaliyodhihirika wakati wa uchaguzi ni wananchi kukosa uelewa wa haki zao kama wapigakura pamoja na wajibu wao.

Suala la elimu ya mpigakura lina umuhimu mkubwa, ingawa huko nyuma halikupewa uzito mkubwa kama ambavyo sasa NEC imeamua kufanya kwa kwenda katika halmashauri ambazo ndiko wanakoishi wananchi.

Kimsingi, hatua hiyo inamaanisha kwamba maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 yameanza.

Tunakubaliana na kauli ya Kailima kuwa hiyo ni fursa ambayo wananchi kwa muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo tunawashauri wafuatilie kupitia redio za kijamii kwenye halmashauri ili waelimike kuelimika zaidi.

Kikubwa ambacho tunaamini kuwa mpango huo utawanufaisha wananchi ni kupunguza kama sio kumaliza manung’uniko ya kura ambayo yamekuwa yakijitokeza wakati wa uchaguzi sambamba na kuwezesha kuwapo na uchaguzi mzuri zaidi.

Jambo la kufurahisha ni kuwa wananchi watapatiwa fursa ya kuelewa mada zitakazotolewa na NEC kutokana na kuwapo utaratibu wa kuuliza maswali na kupewa majibu na wawasilishaji.

Changamoto kwa wadau na wananchi ni kujitokeza kusikiliza mada hizo kwa kuwa zinazungumzia masuala yote muhimu, hivyo ukizisoma na kuzisikiliza ataelewa mfumo mzima wa masuala ya kupiga kura.

Pamoja na kuipongeza Tume kwa kutekeleza mpango huu wa kutoa elimu ya mpigakura sehemu zote nchini, ushauri wetu ni kuwa mpango huu uwe endelevu kwa kuwa kila wakati kunakuwa na wapigakura wapya, ambao wanahitaji uelewa wa mambo muhimu katika upigaji kura.

Ingawa halmashauri nyingi zina redio za kijamii zitakazowawezesha wananchi wengi kufuatilia na kushiriki katika mpango huo, lakini tunaishauri NEC kuangalia uwezekeno wa kushirikiana na wadau katika utoaji wa elimu hiyo ili Watanzania wengi zaidi wafikiwe na wanufaike.

Tunaona ushirikishaji wadau ni njia bora zaidi kwa kuwa elimu ya mpigakura inaweza kutolewa katika maeneo ya mijumuiko ya watu kama mikutano ya ndani na ya hadhara, makongamano, warsha na midahalo.

Matarajio yetu ni kuwa hatua ya kutoa elimu kwa mpigakura kwa kutumia redio za kijamii itasaidia kuwezesha wananchi wengi kujua mambo muhimu katika uchaguzi, hivyo mchakato wa uchaguzi ujao utakapoanza itakuwa rahisi kuelewa haki na wajibu wao na matokeo yake uchaguzi utakuwa bora kutokana na kutokuwapo manung’uniko mengi kama ilivyo sasa.