Elimu ni muhimu, siyo kutoza faini barabarani

05Oct 2016
Mhariri
Nipashe
Elimu ni muhimu, siyo kutoza faini barabarani

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, limekusanya Sh. milioni 464.790 kutokana na makosa mbalimbali ya vyombo vya usafiri 29,499 vilivyokamatwa ndani ya siku saba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro, vyombo hivyo vilikamatwa na kutozwa faini hiyo kutokana na makosa 15,493 yalivyokutwa nayo.

Kamanda Sirro alisema idadi ya magari ni 14,006, pikipiki 1,487, daladala 4,765, magari binafsi na malori kwa ujumla yakiwa 9,241 pamoja na bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu (helment) na kupakia mishikaki ni 15,493.

Kiasi cha fedha kilichokusanywa ni kukubwa na kinachangia katika mapato ya serikali. Jeshi la Polisi kwa upande wao ni mafanikio kwa kuwa kukusanya mapato ya kutosha kutokana na makosa ya vyombo vya moto barabarani kwao ni kutimiza malengo waliyopangiwa. Kuna taarifa pia kwamba askari wanaotimiza malengo ya ukusanyaji wananufaika kwa kupewa motisha.

Pamoja na makusanyo hayo, sisi tunaona kwamba sio sahihi kwa serikali na jeshi hilo kuelekeza nguvu na mikakati katika kukusanya fedha zitokanazo na makosa ya barabarani.

Lengo la kuwa na Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo usalama wa raia barabarani ni jukumu la msingi; kwa maana ya kudhibiti ajali sambamba na kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wa barabara.

Udhibiti wa ajali za barabarani haupaswi kujikita tu katika kuwatoza faini wanaokiuka sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani, isipokuwa jeshi hilo kupanga mikakati na kutumia muda wa kutosha kutoa elimu kwa kuwa ajali nyingi zinachangiwa na madereva wengi na watumiaji wa barabara kutokuwa na uelewa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani ambayo ilizinduliwa Septemba 26 na kufikia kilele Oktoba Mosi ilikuwa inasema ‘Hatutaki Ajali, Tunataka Kuishi’, Kaulimbiu hiyo ilitokana na kuongezeka kwa kasi kwa ajali za barabarani na kusababisha vifo vingi na kuwaacha watu wengine wakipoteza viungo vyao.

Hatutaki kurejea katika takwimu za kutisha za maelfu ya vifo na majeruhi kwa miezi saba tu ya mwaka huu, lakini itoshe kusema kwamba hali ilivyo kwa sasa inahitaji juhudi za makusudi za kupunguza ajali za barabarani kama sio kuzikomesha kabisa.

Hatua ya kujielekeza katika kukusanya fedha za faini na kuacha kutoa elimu kwa madereva na jamii ni ishara tosha kwamba bado kuna tatizo kubwa ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi, vinginevyo ajali zitaongezeka.

Wakati mwingine inashangaza kuona madereva wanaoendesha magari wakiwa wamelewa wakitozwa faini tu badala ya kuelimishwa athari za kutumia vileo na kuendesha. Elimu ingewasaidia kutambua umuhimu wa kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vileo.

Tunaamini kwamba kama askari watajikita kwenye utoaji wa elimu zaidi, kutakuwa na mabadiliko makubwa na ajali ambazo kwa sasa zimekuwa tishio kwa maisha ya Watanzania zitapungua kwa kiwango kikubwa.

Hatupingi faini kwa wanaokiuka sheria za barabarani, isipokuwa tumaanini kuwa elimu ni muhimu zaidi na itasaidia kupunguza makosa.

Kadhalika, tunashauri kuwapo utaratibu wa kukagua magari hususani mabasi mara kwa mara badala ya kusubiri wiki ya nenda kwa usalama mara moja kwa mwaka.

Habari Kubwa