Elimu sahihi chanjo ya Covid-19 itolewe

06Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Elimu sahihi chanjo ya Covid-19 itolewe

JANA serikali ilitangaza mwongozo kwa shule za msingi, sekondari na vyuo katika kipindi hiki cha corona, na pia imeeleza kuwa chanjo itakuwa bure, huku kukiwa na mikakati ya kuwa na kiwanda cha kutengeneza chanjo hiyo nchini.

Hii ni habari njema kwa kuwa wapo waliokuwa wanahofia gharama za kupata chanjo hiyo, na sasa imepitishwa kuwa ni bure hakutakuwa na gharama zozote.
 
Uamuzi wa serikali kutoa chanjo hizo bure na kuweka mikakati ya kujenga kiwanda nchini, ambacho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 80 ni wa kupongezwa.
 
Jitihada hizi za serikali ni za kuungwa mkono kwa kuwa zina kwenda kuhatarisha upatikanaji wa huduma hiyo, ambayo ni hiari kwa kila Mtanzania.
 
Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusiana na chanjo hiyo nchini, ambazo zinaupotoshaji mwingi kiasi cha kuwachanganya wananchi na wengi kuondoa imani juu ya chanjo hiyo na kuanza kuikataa kabla hajaiingia nchini, na hasa kuwapo kwa taarifa za madhara.
 
Kuna taarifa nyingi ikiwamo muda wa chanjo kuanza kutumika baada ya kutengenezwa, bado haijapitishwa na mamlaka za kimataifa na kuna madhara yaliyoainishwa kwa kila chanjo.
 
Lakini kuna baadhi ya nchi zimesema aina fulani ya chanjo inayotumika nchi fulani raia wake hawataruhusiwa kuingia nchi za bara fulani, na kutaka chanjo ya nchi fulani kutumika kwa watu wanaotaka kuingia katika nchi hizo.
 
Ni muhimu elimu kwa umma ikatolewa kikamilifu ili kuondoa upotoshaji mkubwa unaoendelea, kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa chanjo hiyo kwa manufaa yao, kwa kuwa kati ya chanjo zote zipo ambazo ni nzuri na zimethibitishwa na wengi.
 
Ni muhimu pia kukawa na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma kuhusiana na chanjo, ambazo serikali imeamua kuziingiza nchini baada ya kuridhishwa nazo.
 
Kwa wale ambao wameshapata chanjo hiyo kwenye mataifa mengine na kuna uthibitisho wake, ni muhimu wakatumika kuelimisha umma kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ili kuisaidia jamii kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala hayo.
 
Wapo ambao bila kujali taarifa zilizopo wanataka chanjo hiyo, na wenye uwezo wameshaenda nje ya nchi na kuchanjwa na wanaendelea na shughuli zao.
 
Pia kwa sasa nchi imethibitisha kuna wimbio la tatu la corona, ni muhimu kutoa elimu na kuongeza uangalifu hasa kwenye maeneo yenye mikusanyiko.
 
Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha mfano kwa kuhakikisha kwenye mkusanyiko wowote anavaa barakoa, hii ikiwa ni kutuma ujumbe kwa umma kuwa lazima wananchi wavae barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
 
Bado hatua hazijachukuliwa kwa usafiri wa umma kuhakikisha wananawa mikono muda wote, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
 
Kwa sasa shule za msingi na sekondari zimefunguliwa na serikali imehuisha mwongozo wa corona uliotolewa mwaka jana, ambao unataka kuwapo maji tiririka na sabuni, uvaaji wa barakoa na kuchukua hatua za haraka kwa wanaoonekana kuugua.
 
Ni muhimu utaratibu wa kunawa na kuvaa barakoa kwa wanafunzi kutegemea na umri na taratibu za kiafya, kufanya hivyo kwa usahihi ili kusaidia Watanzania kujikinga na ugonjwa huo.
 

Habari Kubwa