Elimu ya mikopo sawa, lakini HESLB ipanue wigo wanufaika

17Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Elimu ya mikopo sawa, lakini HESLB ipanue wigo wanufaika

TAARIFA kwamba Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imeanza kuendesha programu za elimu kuhusu uombaji wa mikopo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu ambao wapo katika kambi 17 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini, ni hatua ya kuungwa mkono.

Programu hizo ni mwendelezo wa programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi ambazo HESLB iliziendesha mwezi Aprili na Mei, mwaka huu katika shule 119 za sekondari zilizopo kwenye mikoa 17 na kuwafikia wanafunzi 27,913 waliokuwa wanajiandaa na mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita iliyomalizika mwishoni mwa mwezi Mei, mwaka huu.

Akizungumza juzi katika kambi ya JKT Ruvu, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema lengo la programu hizo ni kuwawezesha wanafunzi kuomba mikopo kwa usahihi na hatimaye wenye sifa wapate mkopo na elimu ya juu.

Alisema kwa  kushirikiana na wadau wao, likiwamo JKT, HESLB imedhamiria kuwafikia wahitaji wa mikopo pale walipo, ndiyo sababu walikwenda kambini hapo na kambi nyingine kama 16.

Mkakati huo wa HESLB  tunaona kuwa una lengo zuri kutokana na huko nyuma mchakato wa uombaji wa mikopo kuonekana na vikwazo kwa waombaji wengi hususan vijana ambao wanakuwa wamehitimu kidato cha sita.

Kukosekana kwa elimu katika mchakato wa uombaji wa mikopo kumekuwa kukisababisha vijana hao kukosa kwa sababu tu waliomba bila kufuata taratibu sahihi, hivyo wengi kujikuta mwisho wa siku wakikosa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Bodi ya Mikopo iliweka vigezo mbalimbali ambavyo kila mwombaji anatakiwa kuvikidhi, hivyo kuanzisha na kutekeleza programu ya elimu ya kuomba mikopo ni ishara kwamba imedhamiria kuwasaidia waombaji ili wasikwazike.

Pia hatua ya kuwafuata wahitimu wa kidato cha sita ambao wako kwenye kambi za jeshi, unawarahisishia kuomba mikopo kwa usahihi. Hii ni kwa sababu wasingepata msaada kulinganisha na wale waliohitimu masomo bila kupita JKT.

Mbali na kuipongeza HESLB kwa kubuni na kutekeleza programu hiyo, tunashauri elimu hiyo iwe endelevu shuleni kwa wanafunzi ambao wanatarajia kuhitimu na waliopitia kwenye kambi za JKT.

Wahitimu ambao hawapitii JKT angalau wanakuwa na fursa ya kupata msaada kwa watu wengine wenye uelewa katika kujaza fomu za maombi kwa usahihi.

Kwa mwaka ujao wa masomo tunaishauri Bodi ya Mikopo iendelee kuboresha mazingira ya utoaji wa mikopo ili walengwa wengi wanufaike na kusoma bila changamoto.

Kumekuwapo na dhana kuwa vijana waliosoma shule za binafsi hawana haki ya kupata mikopo kwa madai kuwa wazazi na walezi wao wana uwezo kiuchumi.

Hata hivyo, kiuhalisia dhana hii haina ukweli kwa kuwa kuna wazazi na walezi ambao baadaye wanaathirika kiuchumi, hivyo kukosa uwezo wa kuwasomesha wategemezi wao.

Aidha, wapo baadhi ya wazazi na walezi ambao wanawasomesha wategemezi wao katika shule binafsi, lakini wanapostaafu nguvu zinapungua sambamba na kipato, hivyo, kuwa vigumu kwao kugharamia elimu ya juu.

Katika mazingira haya, tunaona kuwa kuna sababu za msingi kwa HESLB kuachana na dhana hii, badala yake ifuatilie kwa karibu ili waombaji wa aina hii wapatiwe mikopo kwa kuwa ni haki yao kama Watanzania wengine.

Habari Kubwa