Fao kukosa ajira siyo msaada, lipo kisheria

18Apr 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Fao kukosa ajira siyo msaada, lipo kisheria

KATIKA gazeti la jana tulichapisha habari kuhusu malalamiko ya baadhi ya wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kupigwa danadana ya kulipwa fedha za mafao ya upotevu wa ajira na michango yao ya kujitoa uanachama kwa muda mrefu bila mafanikio.

Wanachama hao walitoa madai yao jinsi ambavyo wamekuwa wakisumbuliwa na mwisho wa siku wamebaini kwamba wote wamekuwa wakiambiwa yanayofanana ya kucheleweshewa kulipwa mafao hayo.

Miongoni mwa majibu hayo ya pamoja ni wanachama hao kuelezwa kuwa walikosea kuweka alama ya dole gumba, kuwapo kwa tatizo la mtandao na wanasimika mfumo mpya kwa kushirikiana na Hazina.

Wanachama hao wameitaja ofisi ya NSSF Ubungo, jijini Dar es Salaam ndiyo imekuwa ikiwasababishia usumbufu kila siku wa kupewa sababu mpya za kuchelewa kulipwa haki yao kisheria.

Mmoja wa wanachama hao alibainisha kuwa mkataba wake wa kazi ulikwisha tangu Julai mwaka 2018, alifungua maombi ya malipo na ilipofika Novemba mwaka huo.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo licha ya kupokelewa alijibiwa kwamba hawezi kulipwa michango yake yote, badala yake alitakiwa kufungua fao la upotevu wa ajira ambalo alifungua Desemba 11, mwaka huu, lakini ajabu ni kwamba hadi juzi hakuwa amelipwa chochote.

Tunatambua hali ya maisha inavyokuwa ngumu hasa kwa mtu ambaye alikuwa ni mwajiriwa, alikuwa na uhakika wa kipato, lakini sasa anaweza kuishi wa kubahatisha, kwa hiyo ni wazi mwanachama huyo na wenzake kadhaa wamejikuta kwenye wakati mgumu.

Kucheleweshwa kulipwa kwa mafao hayo ni jambo ambalo limetushangaza kwa kuwa inazidi kuwaongezea ugumu zaidi wa maisha kwa kuwa uifuatilia kwa karibu unaweza kubaini wana madeni yamewaelemea ambayo mengine yameongezwa na gharama za nauli wanazotumia kufuatilia madai yao.

Tunafahamu kwamba fao la kukosa ajira halitolewi kama msaada, bali lipo kwenye sheria mpya ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kuunganishwa kwa baadhi ya mifuko hiyo, hivyo wana haki kabisa ya kulipwa kama ilivyoelekezwa.

Awali kabla ya sheria hiyo hakukuwa na fao hili la kujitoa, badala yake wanachama walijitoa kwenye uchangiaji walipopoteza ajira kisha wakarejeshewa amana zao hatua hii haikuwa kisheria.

Wanachama waliaminishwa kuwa fao la kutokuwa na ajira ni zuri, kwa kuwa mwanachama anaanza kupewa pensheni ya kutokuwa na ajira pale anapowasilisha maombi kwa mfuko husika ndani ya wiki sita.

Sheria hiyo inautaka mfuko husika kushughulikia maombi ya mwanachama ndai ndani ya wiki sita, baada ya kukamilisha atakuwa anapewa asilimia 33.3 ya mshahara wake wa mwisho kwa kipindi cha miezi sita.

Tunatamani tuone mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwa ni faraja kwa wanachama wake kwa kuhakikisha wanapata haki zao za msingi zinazoainishwa na sheria mpya, likiwamo fao la kujitoa ambalo tunaamini linaweza kumsaidia kumsogeza kujipanga upya katika kujitafutia kipato.

Tunawasihi viongozi husika kuona umuhimu wa kuwasimamia watendaji wa mifuko hiyo kuhakikisha wanachama wanalipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria, badala ya kuwa wasumbufu na kuwafanya wajute kuwa wanachama wao.

Kikukwa ikumbukwe kuwa wahusika licha ya kukosa ajira na kukumbana na hali ngumu ya maisha, bado wanategemewa na familia zao, ikiwamo kutoa huduma za msingio za elimu na matibabu kwa watoto wao na wategemezi, kwa kutaja baadhi.

Katika kusimamia haki za wanyonge, serikali isikubali wananchi wake hao wakateseka kila sababu za msingi.

Habari Kubwa