FCC isaidie mchakato mabadiliko Simba SC

23Nov 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
FCC isaidie mchakato mabadiliko Simba SC

WANACHAMA na mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla wanatamani kuona mchakato wa mabadiliko Simba unakamilika na klabu hiyo kuendeshwa kwa mfumo mpya wa hisa, ambao utasaidia kukua kwa soka si la klabu pekee, bali la Tanzania kwa ujumla.

Hata hivyo, baada ya siku chache zilizopita Mwenyekiti ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed "Mo" Dewji, kueleza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo bado upo mikononi mwa Tume ya Ushindani (FCC), wiki iliyopita tume hiyo iliibuka na kufafanua mambo kadhaa pamoja na kukanusha kuwa wao si kikwazo cha kuchelewa kwa mabadiliko hayo.

Katika taarifa hiyo, FCC ilieleza kufanya uchambuzi wa awali wa maombi ya Simba Sports Club Company Limited ya kupatiwa mwongozo wa kisheria chini ya Sheria ya Ushindani kuhusu namna ya kushughulikia mchakato wa mabadiliko unaohusisha Kampuni za Simba Sports Club Holding Company Limited, Mo Simba Company Limited, Simba Sports Club Company Limited na Klabu ya Simba.

Na baada ya hapo, FCC ilieleza kufanya vikao viwili kati yake na Simba Sports Club Company Limited hadi Julai 24, 2020 na wadaawa (wapeleka maombi) kuelewa mwongozo wa kisheria na kuahidi kuutekeleza kama walivyoelekezwa.

Yapo mambo mengi ya msingi FCC, imeyafafanua ambayo wadaawa walipaswa kuyatekeleza, lakini ikumbukwe mfumo huu wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ndiyo kwanza unaingia katika soka letu na Afrika Mashariki kwa ujumla, hivyo ni mchakato unaohitaji ushirikiano wa kila upande ili kuuwezesha kwa faida ya soka letu.

Kama ambavyo, Simba ilianza awali kwa kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambacho ni chombo kingine cha serikali, tunatambua yapo maelekezo mengi ambayo ilipewa ikitakiwa kuyatekeleza wakati huu ikiendelea na mchakato huo.

Hata hivyo, kinachoonekana kwa sasa ni kuwapo kwa baadhi ya taratibu ambazo pengine wadaawa walitekeleza kulingana na maelekezo kutoka BMT wakati huo huo, kwa FCC kwao yakionekana kama ni ukiukwaji wa sheria kabla ya hatua ambayo mchakato huo umefikia.

Mfano ni hatua ya FCC kutaka ufafanuzi kuhusu uteuzi wa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu ya Simba kabla ya uwekezaji kufanyika, suala ambalo kwa upande wa wadaawa wametumia mabadiliko ya katiba yao ikiwamo maelekezo ya BMT kwa kuwa na kipindi cha mpito kwani klabu inaendelee kushiriki kalenda mbalimbali za ligi na haisimami ili kusubiri mchakato huo kukamilika.

Si lengo la Nipashe kusimama upande wowote katika mkanganyiko huu, kwani kwa namna tulivyofuatilia hatua kwa hatua, tunaamini tofauti ama utata unaojitokeza katika kukamilika kwa mchakato huo, zinatokana na mwingiliano wa kanuni zinachongiwa na ugeni wa suala la mabadiliko kwa klabu ambayo ilikuwa ikiendeshwa na wanachama.

Hivyo, kuna haja kubwa ya pande zote zinazohusika ikiwamo BMT kuketi pamoja na pale ambapo kuna ukiukwaji wa kanuni, wadaawa kupewa muongozoo na kurejeshwa kutekeleza/kurekebisha badala ya kuendelea kuchelewesha ama kusitisha mchakato huo.

Sisi tunaamini endapo mchakato huo wa mabadiliko utakamilika, klabu nyingi nchini zitafuata mfumo huo na ndipo soka letu litapiga hatua na kufika kule ambapo tulikuwa tukipatamani/kupahitaji kwa muda mrefu.

Hakuna ubishi kuwa, soka ni ajira kubwa kwa vijana nchini na ili kupiga hatua ama kupata maendeleo lengo kupitia sekta hiyo, kunahitaji uwekezaji mkubwa, hivyo hiki ni kipindi cha serikali kutoa sapoti kubwa kwa namna yoyote ile katika kufanikisha mchakato huo wa mabadiliko.

Tunatamani kuona ligi ya Tanzania ikiwa bora zaidi Afrika na pengine miongoni mwa ligi bora duniani ambazo zitavutia wawekezaji wakubwa zaidi kutoka nje, na ili hilo lifanikiwe,
serikali inapaswa kusimamia kwa umakini mwanzo huo wa mchakato wa mabadiliko Simba ili kufanikiwa na hatimaye klabu zingine kufuata njia hiyo kama ambavyo Klabu ya Yanga nayo imeanza.

Habari Kubwa