Fedha ziongezwe mikopo ya wanafunzi mwakani

16May 2017
Mhariri
Nipashe
Fedha ziongezwe mikopo ya wanafunzi mwakani

KUTOKANA na Serikali kutenga fedha zisizotosheleza mahitaji ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka ujao wa fedha, Bunge limeishauri serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Ombi hilo limetokana na kubainika kuwa wanafunzi wengi watakosa fedha hizo katika mwaka ujao 2017/18 kutokana na bajeti ndogo iliyotengwa.

Ushauri huo ulitolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipokuwa ikiwasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo , alisema wamebaini wanafunzi wengi watakosa mikopo mwaka ujao wa fedha licha ya kuwa na ufaulu mzuri.

Alisema mwaka huu wa fedha wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa ukamilifu, lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo, hivyo kuacha wengine 22,947 bila mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni 427.5 kutotosheleza mahitaji.

Bashe alisema mwaka ujao wa fedha HESLB imeombewa Sh. bilioni 427.5 (sawa na bajeti ya mwaka huu) wakati ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka huu.

Ushauri wa kamati hiyo unapaswa kufanyiwa kazi na serikali kwa kuzingatia kuwa suala la elimu ya juu ni nyeti na linagusa watu wengi hususani ambao wana sifa na vigezo vya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Kigezo cha kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi ni sababu muhimu ya Bunge kuishauri serikali kutafakari na kufanya uamuzi wa kuongeza bajeti ya HESLB katika mwaka ujao wa fedha ili wanafunzi wenye sifa wakopeshwe kusoma masomo ya elimu ya juu.

Itakumbukwa pia kwamba suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu, ingawa tunajua kwamba katika miaka ya karibuni serikali iliweka vigezo vipya katika utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo.

Tunaelewa kuwa uwezo wa serikali kifedha ni mdogo kutoa mikopo kwa waombaji wote na ndiyo maana utaratibu mpya unatoa kipaumbele kwa baadhi ya masomo hususani ya sayansi, tena kwa wanafunzi ambao wazazi na walezi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.

Kiuhalisia, mahitaji ya mikopo kila mwaka lazima yaongezeke kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya ongezeko la idadi ya watu ambalo pia linasababisha ongezeko la wanafunzi wa elimu ya juu.

Kutokana na hali hiyo, serikali inapaswa kuhakikisha kwamba inajitahidi kuhakikisha kuwa bajeti ya HESLB inaongezeka ili waombaji wote wanaokidhi vigezo wanakopeshwa.

Kutokana na takwimu kuonyesha kuwapo kwa ongezeko kubwa katika makusanyo ya mapato ya serikali kila mwezi, tunaona kuwa ipo haja kwa serikali kuangalia upya uwezekano wa kupanua wigo katika suala zima la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Umuhimu huo unatokana na taratibu zinazotumika sasa kuwakosesha mikopo waombaji wengi ambao licha ya kuonekana kuwa wazazi na walezi wao walikuwa na uwezo miaka ya nyuma kutokana na kuwasomesha shule za binafsi kutokuwa na uwezo huo tena.

Tunaishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu maalum wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuiwezesha HESLB kuwa na uwezo wa kukopesha wanafunzi wengi zaidi kila mwaka.

Tunaamini hilo litafanyika kutokana na hofu iliyokuwapo dhidi ya HESLB kumalizika kutokana na serikali kufuatilia utoaji mikopo, urejeshaji na kudhibiti mianya ya wizi na ufujaji wa fedha katika bodi hiyo.