Filamu inayomshirikisha Rais suluhisho bora utata tanzanite

07Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Filamu inayomshirikisha Rais suluhisho bora utata tanzanite

TANZANIA ina neema ya utajiri wa aina nyingi, kuanzia madini ya vito vya thamani kama dhahabu, almasi hadi tanzanite, isiyopatikana kwingine kokote duniani.

Usafirishaji na uuzaji wa tanzanite unaofanywa na baadhi ya majirani wa Tanzania na baadhi ya nchi za mbali zikiwamo kutoka Bara la Asia, umekuwa ukiendana na upotoshaji dunia, hata baadhi wakaaamini madini hayo si ya nchi hii.

Hali hiyo kwa namna moja au nyingine, imesababisha nchi kukosa fedha za kigeni ambazo zingetokana na uuzaji wa madini hayo sehemu mbalimbali duniani, hasa ikizingatiwa ukweli kwamba yana thamani kubwa.

Kutokana na hali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, ameshajitoa kimasomaso kuchukua hatua ambazo huenda zitamaliza utata wa upotoshaji huo wa muda mrefu, kuhusu tanzanite, kwamba isijulikane kuwa inapatikana kwa upekee nchini Tanzania.

Anachokifanya Rais Samia kwa sasa, ni kushiriki utengenezaji filamu itakayoonyesha mazuri yaliyopo nchini. Alishaanza kwenye mgodi wa Mirerani, wilayani Simanjiro mwishoni mwa wiki iliyopita, akinuia kuionyesha dunia tanzanite ni ya Tanzania, kama jina lake linavyoashiria.

Yeye na timu yake wamekwenda kwenye machimbo, wanachukua picha namna madini yanavyochimbwa, inavyopimwa, inavyoongezwa thamani hadi pale vinapopatikana vito vya madini hayo.

Kwa mujibu wa Rais, sasa wale wanaouza ovyo huko nje ya nchi, wajue kuwa ni madini yatokayo Tanzania na kwamba hata dunia nayo ithamini uhalisia ulioko, kwa kuwa yeye na timu yake wanaonyesha ilivyo.

Tunaamini kuwa hatua hiyo ya serikali itaisaidia dunia kujua ukweli kuhusu sehemu yanakotoka madini hayo, kuliko ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya wapotoshaji kimataifa kwamba tanzanite haitoki kwetu.

Kimsingi, Tanzania ina vivutio vingi vikiwamo mbuga za wanyama ambazo watalii hupenda kuzitembelea na sasa Rais Samia ameamua kujitosa kimasomaso kutangaza vivutio vyote vya nchi hii kupitia filamu. Ni uamuzi unaopaswa kupigiwa makofi na kila mtu.

Jamii sasa inaona kuwa ni wakati mwafaka wa dunia kujua Tanzania ilivyo kuanzia utajiri wake wa madini, hadi vivutio vilivyomo, ili watalii waje kwa wingi na kuifanya nchi ipatwe fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya maendeleo yake.

Ni matarajio yetu kwamba uandaaji filamu hiyo, pia utasaidia kuondoa utata wa muda mrefu kuhusu ulipo Mlima Kilimanjaro ambao baadhi ya watu nje ya nchi wanadhani haupo Tanzania.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya watu walioko mbali wamekuwa wakiamini mlima huo upo katika nchi jirani hata kuinyima nchi watalii, hali inayosemekana ni zao la baadhi ya zinazolazimisha kuchangamkia fursa zisizo za kwao.

Hatua ya kutengeneza filamu hiyo, tunaichukulia kama suluhisho la utata ambao umekuwapo muda mrefu hasa kwenye madini ya tanzanite, hali kadhalika Mlima Kilimanjaro, ukipotoshwa sio mali ya Tanzania.

Kwa mwendo huo, tunaona wazi sasa dunia itajua ukweli jinsi Tanzania ilivyo na utajiri wa madini ya kipekee, pia vivutio vya asili hata wawekezaji kuja nchini kwa ajili ya miradi mbalimbali kama ya uchimbaji, hata kushuhudia vivutio vya kitalii.

Hivyo, wito wetu ni kuwataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizo za Rais Samia kwa lengo la kujipatia fedha nyingi za kigeni, kwa kutumia madini na vivutio vilivyopo kunufaisha maendeleo ya nchi.

Habari Kubwa