Funzo la corona kwa sekta ya afya

20Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Funzo la corona kwa sekta ya afya

POLENI Watanzania kwa hofu ya homa ya corona ambayo inamfanya kila mmoja kuwa na woga kutokana na ugonjwa huo unaoua kwa muda mfupi.

Uwapo wa corona umekuja wakati ambao kila mmoja anatakiwa kuwajibika, lakini zaidi sekta ya afya ambayo ina wajibu mkubwa wa kipekee kusimamia na kuhakikisha ulinzi na usalama wa afya kwa wananchi wote.

Tunasema haya kwa sababu ina jukumu kubwa la kuboresha mifumo ya afya na kuweka mikakati ya kudhibiti maambukizi na kutibu wagonjwa.

Tunaona kuwa huu ni wakati pia wa kuhakikisha kuwa kuna fedha za kutosha za kudhibiti tatizo hilo la kuwafikia watu wote bila kujali wanaishi mjini au kijijini.

Kuwapo kwa maradhi haya kunahitaji na kuulazimisha uongozi wa kitaifa kuwa na ridhaa ya kisiasa ya kutumia rasilimali kuanzia fedha, wataalamu na muda na vifaa kutibu na kuokoa maisha ya watu wasidhuriwe na corona.

Tunafurahishwa na hatua na nia ya serikali ya kudhibiti ugonjwa huu kwa kufunga vyuo vikuu na vya kati, shule na kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa isiyo na sababu na pia kuboresha mifumo ya afya na kujitahidi kukabiliana kwa nguvu zote na maradhi haya.

Kwa ujumla, tunaona kuwa funzo linalotokana na corona ni la kipekee na hasa kuona umuhimu wa kuboresha miundombinu ya afya ikiwamo kujizatiti kuwa na huduma na wataalamu wa kutosha ndani ya hospitali zetu kuliko kutegemea na kuamini kuwa matibabu bora yanapatikana nje ya nchi.

Funzo linalotokana na corona ni kwamba haiwezekani kuwapeleka wagonjwa wa maradhi hayo nje ya nchi kwa matibabu. Kama vile kuwapeleka Afrika Kusini, Ulaya au India.

Kwa hiyo, kama ambavyo Tanzania imefanya bidii kuimarisha sehemu kubwa ya sekta ya afya kwa kuanzisha vitengo vya matibabu ya moyo, saratani, mifupa na mishipa ya fahamu pamoja na figo, ndivyo sasa taifa linapaswa kujivunia na kutembea kifua mbele kuwa kila jambo linawezekana iwapo tutatia nia.

Halikadhalika pamoja na juhudi hizo tunapenda kuishauri serikali kufikiria uwezekano wa kuanzisha kitengo maalumu cha magonjwa ya dharura.

Tunashauri haya kwa sababu ukanda wa Afrika umekuwa na magonjwa ya dharura na hatari kama ulivyokuwa mlipuko wa homa ya ebola, dengue, chikungunya na sasa corona.

Tunaamini kuwa kwa kuwa na kituo kama hicho kuna uwezekano wa kudhibiti kwa urahisi lakini pia kuwa na uwezo wa kupunguza ukubwa wa tatizo kwa kuwa kituo kitakuwa na fedha za kutosha, wataalamu kuanzia wauguzi, madaktari, wataalamu wa maabara zikiwamo zinazohamishika (mobile laboratories), vifaa kama magari, helkopta, droni na vifaa tiba ikiwamo hadubini za kisasa zaidi.

Tunaona kuwa kuwapo kwa kituo na wataalamu hao kutasaidia kupunguza ugumu wa tatizo na kufanikisha wepesi katika kukabiliana nalo.

Pamoja na mambo mengine ni wazi kuwa miaka ya nyuma ni kama sekta ya afya ilikuwa zaidi ikihudumiwa na wahisani, lakini tunaipongeza serikali leo kwa kuisimamia kikamilifu sekta hii na kuiboresha kwa kutumia fedha za ndani.

Jitihada hizo zimefanikisha kutafuta na kuongeza fedha kwa ajili ya sekta hiyo, kufunza wataalamu wa kada mbalimbali, kuboresha huduma katika hospitali za wilaya, rufani na hospitali maalumu za kikanda na kudhibiti ukusanya holela wa mapato kwenye huduma za afya ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Tutaendelea kuungana na serikali kupambana na corona kwa kuielimisha jamii kuhusu kujikinga na kudhibiti ugonjwa huu.

Habari Kubwa