Gawio ni mapato muhimu

26Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Gawio ni mapato muhimu

RAIS John Magufuli ametoa miezi miwili kwa viongozi wa mashirika, taasisi na kampuni za umma 187 kutoa gawio kwa serikali na endapo wakishindwa, waondoke wenyewe kwenye nafasi zao.

Kwa utendaji wa Rais Magufuli, ni wazi kwamba kauli yake haitarudi bure. Hapo ndiyo itakapodhihirika kuwa cheo ni dhamana, kwani ni shinikizo la kiutawala litakalowazindua kutoka usingizini, baadhi ya viongozi waliolala.

Tunatambua kuwa pia imewasababishia matumbo joto wale waliokuwa wamejisahau kuwajibika kuhakikisha wanaongoza vyema na kuwezesha taasisi au kampuni hizo zinajiendesha kwa tija na faida.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo juzi Ikulu Chamwino jijini Dodoma, alipokea gawio, michango na ziada kwa mashirika, kampuni na taasisi mbalimbali ambazo serikali ina hisa au inazimiliki.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kupokea gawio, kwani kampuni za simu za TTCL na Airtel. Kampuni zingine ni Puma Energy Tanzania na benki ya CRDB kwa nyakati tofauti zilikabidhi gawio kwa serikali.

Rais Magufuli alieleza kuwa serikali hadi sasa imeshawekeza mtaji wa Sh. trilioni 59.6 kwa mashirika na taasisi 266, ingawa anakiri kuna maeneo ya uwekezaji huo, unakabiliwa na changamoto ya usimamizi na utendaji duni. Alitoa mfano kuwa mwaka 2014/15, serikali ilikusanya Sh. bilioni 130 kutoka mashirika 24 na mwaka 2015/16 zilikusanywa Sh. bilioni 249.3 kutoka taasisi na mashirika 25.

Kutokana na kauli ya Rais Magufuli, tunaamini kuwa kuna ukimya kutoka kwa viongozi wa taasisi hizo, hali ambayo inajenga taswira ya kulegalega kwenda na kazi anayoitaka mkuu huyo wa nchi, ishara mojawapo inayojionyesha kupitia gawio.

Rais alisema tangu aingie madarakani serikali yake imechukua hatua kadhaa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato, akitaja mifano: Mwaka 2016/17 zilikusanywa Sh. bilioni 677 kutoka taasisi 38; 2017/18 zilikusanywa Sh. bilioni 842.13 kutoka mashirika na taasisi 40; na mwaka 2018/19 Sh. trilioni 1.05 kutoka taasisi na mashirika 79.

Mapato ya gawio la taasisi, mashirika na kampuni yameongezeka na kufikia Sh. trilioni 1.05. Mashirika na kampuni 81 yaliyotajwa kuwa ni ya kibiashara, kati yao 40 yameshindwa kutoa gawio kutokana na madai ya kujiendesha kwa hasara.

Nasi tunajiuliza maswali kuwa wakati viongozi wa mashirika hayo 266 yaliyochangia ni 79 na serikali imeshawekeza mtaji wa Sh. trilioni 59.6 mengine yanafanya nini? Kwa haya mashirika 187 yaliyobaki, kuna nini wanapowaona wenzao wanawasilisha gawio lao wanawaza nini?

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, asilimia 70 ya bajeti ya serikali inategemea makusanyo ya ndani, na nusu ya makusanyo yasiyo ya kodi yanatokana na gawio na michango kutoka kwa kampuni, taasisi, wakala na mashirika ya umma.

Kwa maelezo hayo, tunaweza kutambua jinsi gani gawio ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato kwa serikali, ambayo inawajibika kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi kama maji, elimu, afya, barabara na zingine.

Tunapenda kuwakumbusha kuwa kila zama na nyakati zake, hivyo viongozi wenye dhamana waache kuishi kwa mazoea, badala yake wajitume kuhakikisha wanatumikia majukumu yao ipasavyo, ikiwamo taasisi wanazoziongoza zinatoa gawio kwa serikali kwa wakati mwafaka.

Michango na gawio kwa serikali kama vitatolewa wakati mwafaka, kuna uwezekano wa serikali kujiendesha na kutekeleza miradi mbalimbali badala ya kusubiri washirika wa maendeleo, ambao mara nyingi huchelewa kutekeleza ahadi za kusaidia na wakati mwingine kutotekeleza kabisa.

Habari Kubwa