Haraka ya nini Ligi Kuu Bara?

07Nov 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Haraka ya nini Ligi Kuu Bara?

LIGI kuu ya Bara imemaliza nusu msimu jana huku macho na masikio ya wapenzi wa soka yakiwa kwenye viwanja vya Sokoine na Uhuru, ambako vigogo wa michuano hiyo Yanga na Simba walikuwa wakicheza mechi zao za 14 kati ya 15, hata hivyo.

Macho na masikio ya wapenzi wa soka wa Bara yalikuwa kwenye viwanja hivyo si tu kwa sababu Yanga na Simba ndiyo zenye mashabiki wengi zaidi nchini, lakini pia kutokana na nyendo zao msimu huu.

Wakati mabingwa watetezi Yanga wakionekana kuelemewa na uchovu wa mafanikio yao ya msimu uliopita barani Afrika ilipofika hatua ya ligi ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika, Simba ambayo haijapanda ndege kwa miaka mitatu mfululizo ilikuwa haijafungwa msimu huu.

Nyuma ya pazia la kufikiwa kwa nusu ngwe ya mchuano huo wa kutafuta bingwa wa Bara kwa mwaka 2017, hata hivyo, kuna udhaifu mkubwa ambao ni kasi ya shindano lenyewe.

Ligi kuu ya Bara, Nipashe tunafahamu, ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya soka letu kwa maana inapaswa si tu kupika wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa, bali pia kuwa dira ya michuano ya chini kuanzia ligi daraja la kwanza.

Lakini ligi kuu ya Bara hii, kama ambavyo imekuwa ada katika miaka ya karibuni, imemaliza nusu msimu katika muda wa chini ya miezi mitatu tangu kuanza kwake Agosti 20.

Kucheza mechi 15 ndani ya siku 79, Nipashe tunasema, kunaonyesha kuwa ligi kuu ya Bara ni ya mwendo kasi, na katika maana halisi ya dhana hiyo, mwendokasi ni hatari; unaua.

Tangu kuanza kwa shindano hilo kubwa zaidi la soka nchini, timu zimecheza mpaka mechi sita ndani ya mwezi mmoja, na katika nchi ambayo uwezo wa kiuchumi wa klabu nyingi ni wa kibongo-bongo, palikuwa na vyote viwili - kiwango kilichotarajiwa na wachambuzi na matokeo machache ya kushangaza.

Kama tulivyoanza kueleza Nipashe, mwendo kasi ni hatari, na katika soka la Bara, madhara yake yanaweza kuonekana kwa kiwango cha mchezo kuwa chini licha ya kuwapo kwa wadhamini wakubwa kwenye shindano hilo kulinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Kama tulivyotangulia kusema pia, Nipashe, timu 13 kati ya 16 zinazocheza ligi kuu ya Bara ni zenye uwezo mdogo kiuchumi, zinazotegemea fedha za udhamini wa ligi yenyewe na viingilio kujiendesha.

Hivyo kuzipanga timu hizi kucheza mechi sita ndani ya mwezi mmoja, kwa mfano, tunaona Nipashe, kwanza kunadumaza uwezo uwanjani kutokana na kukosa muda wa kufanya mazoezi ya kawaida na ya kuondoa kasoro zilizojitokeza baada ya michezo husika.

Lakini pia, kuzipanga timu hizi kucheza mechi sita ndani ya mwezi mmoja, tunaona Nipashe, kunazihujumu kimapato viwanjani kutokana na ukosefu wa muda wa mazoezi kuzidi kuzifanya ziwe na kiwango ambacho hukimbiza watazamaji.

Hivyo tuchukue fursa hii, Nipashe, kuiomba Bodi ya Ligi, lakini hasa Shirikisho la Soka, kupanga raundi 15 za ligi kuu ya Bara kuchezwa kwa wastani wa siku 105 badala ya 79 za sasa.

Mbali na kupandisha kiwango cha ligi, kucheza raundi moja ya ligi kwa wiki kutafanya pia mchezo huo uwepo kwa mwaka mzima, hivyo kupandisha pia utimamu wa mwili wa wachezaji wa Taifa Stars.

Habari Kubwa