Hatua hii itaisaidia NIDA kutoa huduma kwa ufanisi

14Jul 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua hii itaisaidia NIDA kutoa huduma kwa ufanisi

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imesema kuanzia mwezi huu, itaanza kutoza fedha taasisi zote za umma na binafsi zinazotumia taarifa za mamlaka hiyo kuhudumia wananchi.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geofrey Tengeneza, aliyasema hayo juzi alipozungumza na wanahabari katika Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Alisema kuna wadau ambao wanatumia taarifa za NIDA kutoa huduma kwa wananchi, na kuwa kuanzia mwezi huu, mamlaka hiyo itaanza kutoza tozo kwa taasisi zote za umma na binafsi ambazo zinatumia taarifa zake kuhudumia wananchi.

Miongoni mwa taasisi na kampuni ambazo zitatakiwa kutozwa ni kampuni za simu, NSSF, Mfuko wa Bima ya Afya, benki na wadau mbalimbali ambao ili watoe huduma kwa wateja wao, wanahitaji kupata taarifa kutoka NIDA, hivyo ni lazima kuzilipia ili kuendelea kutoa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, taasisi hizo zinapaswa kuingia mkataba na NIDA ili kupata huduma hizo, vinginevyo taasisi ambazo zitashindwa kutimiza matakwa hayo, zitasitishiwa huduma hiyo mara moja.

Imeeleza kuwa imeshatoa notisi kwa kampuni ambazo hazijaingia mkataba na NIDA kufanya hivyo hadi Julai 31, mwaka huu, ili zikishindwa zisitishiwe huduma.

Kimsingi, hatua hiyo itaisaidia mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi, kwa kuzingatia kuwa huko nyuma ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa kiasi cha kusababisha isuasue katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.
Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikionekana kwa kila mmoja ni ufinyu wa bajeti kutokana na NIDA kutozalisha badala yake kutegemea fedha za ruzuku kutoka serikalini.

Matokeo yake ni kuwa mamilioni ya Watanzania waliomba vitambulisho muda mrefu, lakini hadi sasa hawajavipata, huku wakipewa ahadi zisizo na utekelezaji.

Hata ofisa huyo wa NIDA amefafanua kuhusiana na hilo kwa kusema kuwa utaratibu huo ni maelekezo kutoka kwa serikalini iliyoitaka mamlaka hiyo kuanza kujitegemea kukusanya fedha kutumia utaratibu huo, ili kuondokana na utaratibu wa kupata fedha za matumizi kutoka serikalini.

Tunaona kuwa uamuzi huo wa serikali ni mzuri, ingawa umechelewa kutolewa. Tunasema hivyo kwa kuwa kama ungetolewa mapema leo hii NIDA ingekuwa inajitosheleza kwa bajeti, hivyo kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi.

Kama mamlaka hiyo ingeelekezwa kujitegemea tangu kuanzishwa, ingekuwa na mapato yake kama zilivyo mamlaka nyingine nchini badala ya kutegemea kila kitu kutoka serikalini, zikiwamo fedha za mishahara, ununuzi wa vifaa na matengenezo yake.

Kwa mfano, kwa muda mrefu NIDA imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kukamilisha taratibu zote za kujiandikisha kwa muda mrefu, lakini hawapatiwi vitambulisho kwa maelezo kuwa mashine zimeharibika hadi hapo zitakapotengenezwa au kununuliwa mpya.

Usumbufu huo umekuwa ukiwafanya baadhi ya watu kukosaa imani kwa mamlaka hiyo, huku wengine wakiiona kama haibadiliki badala yake kufanya kazi kwa mazoea.

Huduma ambazo zinatolewa na mamlaka hiyo kwa kampuni na taasisi za umma ni nyingi, hivyo kuna uhakika kwamba itakusanya mapato yatakayoiwezesha kujiendesha na kiasi kingine cha fedha kupelekwa serikalini.

Ushauri wetu kwa NIDA ni kuwa ikubali mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya pamoja na kuwaandaa watumishi wake kuacha mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea.

Habari Kubwa