Hatua hii itarejesha uhakika usafiri majini

19Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua hii itarejesha uhakika usafiri majini

USAFIRI wa abiria na mizigo kupitia majini umekuwa changamoto kwa wananchi wa maeneo kadhaa nchini, kutokana na kukosa vyombo vya uhakika hususani meli.

Maeneo yanayozungukwa na maziwa wananchi wake wamejikuta wakikosa usafiri wa uhakika kutokana na uchache pamoja na uchakavu wa meli hizo.

Kwa mfano, katika Kanda ya Ziwa Victoria kumekuwapo na changamoto zaidi baada ya kupinduka na kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 800. Meli hiyo haikuopolewa, hivyo kusababisha kukosekana kwa meli nyingine mbadala hadi leo.

Hatuwezi kuelezea athari zote katika mikoa yote inayozungukwa na maziwa nchini, lakini itoshe kusema kuwa wakazi wa maeneo hayo wameathirika sana kiuchumi na kijamii.

Wanasiasa kadhaa  kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitoa ahadi za kuboresha usafiri wa majini hasa ununuzi wa meli mpya katika maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika, bila ahadi hiyo kutekelezwa.

Ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuboresha miundombinu ukiwamo ununuzi wa meli mpya katika maziwa yote mwaka 2015, inaonekana kutimia, baada ya kuanza utekelezaji wake.

Kwa wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Mbeya wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa, wanatarajia kuanza kunufaika na usafiri wa meli ya MV Mbeya II ambayo ujenzi wake unatarajia kukamilika Agosti, mwaka huu.

Kwa miaka miwili sasa wananchi wa maeneo hayo, hawana usafiri wa uhakika baada ya meli ya MV Songea iliyokuwa ikitoa huduma katika ziwa hilo, kusitisha safari zake tangu mwaka 2017 kutokana na kuwa na hitilafu.

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abeid Gallus, alisema mapema wiki hii kuwa ujenzi wa meli hiyo umefika asilimia 82.

Ujenzi wa meli hiyo unagharamiwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa Sh. bilioni 9.1 na ina uwezo wa kupakia mizigo tani 200 na abiria 200 kwa wakati mmoja, hivyo kukamilika kwake itasaidia kupunguza tatizo la usafiri kwa wakazi wa mikoa hiyo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la usafiri kwa wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Mbeya kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa wakitumia usafiri wa boti au mashua, lakini hakuna chombo madhubuti kinachofanya kazi ziwani.

Meli hiyo pia itafungua wigo wa biashara kwa nchi za Malawi na Msumbiji, hivyo kuongeza wigo na kibiashara na kuboresha uchumi wa kwa jamii zinazozungukwa na ziwa hilo.

Katika hatua nyingine, wananchi wa Mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani inayozungukwa na Ziwa Victoria, wanatarajia kunufaika meli mpya inayojengwa itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo.

Mbali na meli hiyo mpya, meli nyingine ya MV Victoria inafanyiwa marekebisho na itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 hadi 4,000 na tani za mizigo 200 hivyo kurahisisha usafiri kwa wakazi hao.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya, aliyaeleza hayo wiki iliyopita kwa waandishi walipotembelea bandari hiyo ili kuona miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TPA.

Alisema ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kukamilika Septemba mwakani na itasaidia kuongeza mapato zaidi katika bandari ya Bukoba ambayo licha ya kutokuwapo kwa meli za abiria, yamefika Sh. milioni 60 kwa mwezi kutoka Sh. milioni 29 miaka ya nyuma. 

Tunazipongeza jitihada hizo za utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli ya ununuzi wa meli mpya pamoja na vivuko katika maeneo mbalimbali nchini, ambao tunaamini kuwa umetokana na umakini katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Habari Kubwa