Hatua hizi zitaisaidia nchi kunufaika na madini

08Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Hatua hizi zitaisaidia nchi kunufaika na madini

UKWELI kuhusiana na sababu ambazo zimesababisha umaskini kwa Watanzania na nchi yetu kuchelewa kupaa kwa maendeleo zimezidi kubainika.

Kwa kipindi kirefu watu wengi wakiwamo hata baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wa kitaifa, wamekuwa wakidai kuwa hawajui sababu za Tanzania kuwa nchi maskini, licha ya kuwa na rasilimali lukuki, tena zikiwamo zenye thamani kubwa.

Kiukweli Tanzania ni nchi iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali nyingi zikiwamo madini ya aina zote, mito, maziwa, bahari, wanyamapori, misitu, ardhi yenye rutuba kwa kutaja baadhi.

Mbali na hilo, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika ambazo waasisi wake baada ya Uhuru wa bendera walibuni na kuweka sera, mipango na mikakati mizuri lengo likiwa ni kuipaisha kimaendeleo haraka na kuwafanya wananchi wanufaike na matunda ya kujitawala.

Itakumbukwa jinsi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alivyoona umuhimu wa kuchagua filosofia ya Ujamaa kupitia Azimio la Arusha kama njia ambayo ingeiwezesha nchi yetu kwenda katika maendeleo haraka na kuwanufaisha wananchi wote bila kuwapo matabaka.

Ndiyo maana katika kufikia lengo hilo ilianzishwa mipango ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu na mikakati kama elimu kwa wote, siasa ni kilimo, kuhamisha makao makuu ya nchi na mingine mingi.

Hatua zingine kama kutaifisha njia kuu za uchumi na kuwekwa chini ya dola lengo lake lilikuwa kuwashirikisha wananchi wote katika umiliki wa uchumi ikiwamo kunufaika na ajira. Kwa kiwango kikubwa wananchi wengi walinufaika kwa kupata bure huduma za uhakika za msingi za kijamii kama elimu, afya, maji na zingine.

Hata hivyo, mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani, yalisitisha kasi ya maendeleo iliyotarajiwa baada ya nchi yetu kubinafsisha uchumi kwa kuuza mashirika na kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza.

Uwekezaji huo hususani katika sekta ya madini leo hii ndio unaoiliza nchi kwamba inaibiwa rasilimali hiyo kutokana na kuwanufaisha wawekezaji wenyewe na mataifa yao na kuiacha nchi yetu katika umaskini wa kutupwa.

Kamati mbili zilizoindwa na Rais John Magufuli mwaka huu kuchunguza uchimbaji na biashara ya dhababu nchini zote zilibainisha udhaifu mkubwa katika usimamizi wa madini na jinsi yanayotoroshewa nje na kuwanufaisha wawekezaji badala ya nchi yetu.

Aidha, kamati mbili maalum za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizoundwa na Spika, Job Ndugai, kuchunguza na kutoa ushauri bora kwa serikali kuhusu uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya almasi na Tanzanite nchini, zimebainisha madudu mengi ya udhaifu mkubwa katika usimamizi, ubadhirifu na uzembe.

Kama zilivyobainisha ripoti za kamati za makinikia ya dhahabu, ripoti za kamati maalum za Bunge nazo zimewataja watumishi kadhaa wa serikali waliopewa dhamana ya kulinda na kusimamia rasilimali zetu kutokuwajibika na kusababishia taifa hasara.

Jana baada ya Rais Magufuli kupokea taarifa hizo za Bunge, aliagiza kuchunguzwa kwa watumishi wote waliotajwa katika ripoti hiyo na kuwataka aliowateua kuachia nafasi zao kupisha uchunguzi dhidi yao.

Wajumbe kamati hizo za Bunge wanahitaji pongezi kwa kazi nzuri ya kubainisha ukweli katika uchimbaji wa madini ya almasi na tanzanite jinsi yasivyolinufaisha taifa.

Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuchukua hatua ya kuwataka wateule wake kukaa kando ya nyadhifa zao kwa kuwa itasaidia uchunguzi dhidi yao kutovurugwa. Tunatarajia kuwa ripoti zote za makinikia ya dhahabu na pamoja na almasi na tanzanite mapendekezo yake yatatumiwa na serikali katika kuweka uchimbaji na biashara ya madini hayo kwenye mstari.

Habari Kubwa