Hatua madhubuti zinahitajika sukari kuwafikia wananchi wote

14May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua madhubuti zinahitajika sukari kuwafikia wananchi wote

JUZI, serikali kupitia Wizara ya Kilimo, ilitoa taarifa bungeni kuhusu mwenendo wa biashara nchini, ikiwatoa hofu wananchi kuhusu upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Wizara hiyo kupitia kwa Waziri wake, Japhet Hasunga, ilikiri kuadimika kwa sukari nchini na kubainisha kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo, kuanzia Mei 10 mwaka huu, tayari tani 4,000 za sukari zilikuwa zimeshawasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam, huku shehena ya tani 21,000 ikitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.

Katika taarifa yake hiyo, serikali pia ililitaarifu Bunge kuwa tani zingine 500 kutoka Afrika Kusini, zimeshawasili katika Bandari ya Kasumuru na kutoa mwanga katika utatuzi wa tatizo la uhaba wa sukari nchini.

Kwa mujibu wa waziri huyo, uhaba wa sukari unaoonekana sasa katika maeneo mbalimbali nchini, umesababishwa na mambo makuu matatu ambayo ni pamoja na meli zilizokuwa zimebeba bidhaa hiyo, kufaulisha mzigo katika meli zingine na kusababisha sukari iliyokuwa inaingia nchini kutokidhi mahitaji.

Sababu nyingine ni mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosabishwa na virusi vya corona (Covid-19) na baadhi ya wafanyabiashara kuficha sukari kwa lengo la kufanya ulanguzi.

Katika ufafanuzi wake, Waziri Hasunga pia alibainisha kuwa mahitaji ya sukari nchini ni tani 35,000 kwa mwezi, hivyo zilivyoingizwa tani 40,000 zilizoagizwa nje ya nchi hivi karibuni, waliamini zingetosha kwa kuwa viwanda vya ndani vilikuwa vianze uzalishaji Mei.

Hata hivyo, Hasunga alisema kutokana na mvua kuendelea kunyesha ni kiwanda kimoja tu kilichoonyesha dalili ya kuanza uzalishaji mwisho wa mwezi.

Nipashe tunaipongeza Wizara ya Kilimo kwa kutambua na kukiri hadharani kwamba nchi inakabiliwa na tatizo la uhaba wa sukari na kuanika mikakati ya kulitatua.

Lakini, Nipashe tunaamini hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo kwa sasa hazitakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hilo ikiwa uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini utaendelea kama hali ilivyo sasa na pia mwenendo wa biashara ya sukari.

Ikumbukwe kuwa kuadimika kwa sukari nchini hakujaanza mwaka huu, kumekuwa kukijitokeza mara kwa mara na hatua kadhaa zimekuwa zikichukuliwa huku baadhi ya watendaji, wakiwamo mawaziri, wakiwajibishwa kutokana na ama kusuasua kwa upatikaji wake au kuwapo kwa ulanguzi katika biashara hiyo.

Nipashe tunaamini kwamba, bila kuwa na usimamizi mzuri katika usambazaji, sukari iliyoagizwa kutoka nje ya nchi, haitawafikia wananchi wa maeneo mengi wenye uhitaji kwa kuwa tayari kuna wafanyabiashara ambao wameamua kufanya ulanguzi, hivyo kuna uwezekano mkubwa ikafichwa na kuendelea kuadimika nchini.

Vilevile, tunaamini kuwa bila kuwa na mkakati madhubuti wa kuongeza uzalishaji kwenye viwanda vya ndani, nchi itaendelea kuwa na tatizo la uhaba wa sukari hasa kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na mlipuko wa virusi vya corona uliosababisha madhara makubwa katika sekta ya uchukuzi.

Kwa kutambua hili, Nipashe tunaishauri Bodi ya Sukari na mamlaka nyingine zinazohusika na biashara ya sukari nchini, kuchukua hatua stahiki kuhakikisha sukari inayoingizwa nchini, inasambazwa katika maeneo yote ya nchi ili kuwafikia wananchi, wakati huo serikali ikipanga kuongeza uzalishaji wa ndani wa bidhaa hiyo.

Ni matarajio yetu kuwa tukio hilo la uhaba wa sukari nchini, halitajirudia tena na kuwasababishia wananchi mateso na usumbufu mkubwa; kwa kuamini kuwa mamlaka husika zitahakikisha kuwa kunakuwapo na mipango na mikakati madhubuti ambayo ni endelevu.

Habari Kubwa