Hatua ya HESLB ni ya kupongeza

16Apr 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua ya HESLB ni ya kupongeza

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kuendesha programu za elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari waliopo mikoani ili kuwaelimisha kuhusu sifa na taratibu za kuomba mikopo kwa usahihi.

Hatua hii muhimu imetangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, juzi wakati akizungumza na wanafunzi 1,166 wa kidato cha sita kutoka shule zote 12 za wilayani Maswa, mkoani Simiyu.

Ni hatua muhimu kwa sababu uendeshaji wa programu hizo unalenga kuondokana na changamoto wanazopata wanafunzi wakati wa kuomba mikopo ya elimu ya juu.

HESLB ilianza kuendesha programu hizo katika mkoa wa Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo katika maelezo yake alieleza kuwa programu hiyo imeanzishwa kutokana na maoni mbalimbali ya wadau kuhusu kuzikabili changamoto hizo ambazo zimekuwa ni kero kwa wengi.

Tunatambua kuwa mikopo hiyo hutolewa ili kuwawezesha wanafunzi wengi wanaotoka katika familia maskini kumudu gharama za masomo na malazi, wakati wanapokuwa katika jitihada zao za kutimiza ndoto zao za kufuzu masomo ya fani mbalimbali.

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya waombaji wa mikopo hiyo, hivyo tunaamini kwa elimu hii itasaida kupunguza kama si kuondoa kabisa changamoto zinazosababisha hali hiyo.

Taarifa zilizopo HESLB zinabainisha kuwa waombaji wa mikopo zaidi ya 57,000 ambao walipata udahili vyuoni mwaka wa masomo 2018/2019, maombi zaidi ya 9,000 yalikuwa na upungufu mkubwa.

Sasa katika program hiyo inaonyesha baadhi ya mambo ambayo yalionekana kuwasumbua waombaji wengi ni pamoja na wanafunzi kutoelewa sifa za kuomba mkopo huo.

Hivyo pamoja na mambo mengine sasa kupitia programu hiyo, wamejuzwa pia nyaraka zipi muhimu zinazotakiwa, namna ya kuomba na kuwasilisha kwa usahihi maombi hayo kwa njia ya mtandao.

Pia jinsi gani wanavyopaswa kuzingatia utaratibu na umuhimu wa kurejesha mkopo mara wamalizapo masomo.

Upungufu huo ni pamoja na kukosa nyaraka kama vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho sahihi vya wadhamini, kutosainiwa na waombaji, wadhamini au serikali za mitaa au vijiji.

Tunaamini kwamba wanafunzi husika watahakikisha wanasoma kwa makini mwongozo utakaotolewa na HESLB ambao unaelezea jinsi ya kuomba mkopo huo hatua kwa hatua.

Jambo la kufurahisha ni kwamba HESLB wamechukua hatua hiyo wakati mwafaka kwa kuwa mwezi Mei wanafunzi wa kidato cha sita wataanza kufanya mitihani yao ya taifa ikiwa ni hatua ya kusaka tiketi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Tunawasisitiza HESLB kuvuta kasi zaidi ili kuwafikia wanafunzi wote wenye sifa za kuomba mikopo hiyo, tukiamini kwamba itasaidia kuongeza idadi ya wasomi nchini.

Kuna faida kubwa ya kuongeza wasomi nchini, kwani watasaidia katika kuvuta kasi ya maendeleo kwa kufanikisha hamasa ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kupotoa ujenzi wa viwanda.

Tusipojipanga vyema kwa kuhakikisha tunazalisha wasomi wa kutosha tutaishia kuajiri wageni kwenye viwanda tunavyovijenga, hivyo HESLB vuteni kasi kupambana na changamoto hizo.

Ni matarajio yetu kuwa bodi hiyo itakuwa inachukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa mikopo kama ilivyofanya kwa kutoa elimu hiyo katika shule za sekondari.

Habari Kubwa