Hatua ya mahakama itekelezwe idara zingine

09Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua ya mahakama itekelezwe idara zingine

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande, juzi alisema kwamba mahakimu 11 ni kati ya watumishi 34 wa mahakama waliofukuzwa kazi mwezi uliopita.

Akizungumza wakati akipokea taarifa za usikilizwaji kesi tangu Januari hadi Agosti 31, Jaji Chande alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ndiyo mamlaka ya nidhamu na ajira kwa wafanyakazi wa mahakama, ilitoa uamuzi huo kwenye kikao chake kilichofanyika Agosti 18.

Kwamba kikao hicho kilishughulikia tu masuala ya nidhamu, na mahakama ilifikia uamuzi wa kuwafukuza kazi wafanyakazi 34, 11 ni mahakimu na 23 ni maofisa wengine wa mahakama.

Kimsingi makosa waliyoyafanya mahakimu waliofukuzwa ni ya kukiuka maadili kwa kuwa Jaji Mkuu alisema mmoja alitumia muhuri wa mahakama kinyume cha taratibu kwa lengo la kujinufaisha na mwingine alifungua kesi ya mirathi bila kuwa na cheti cha kifo. Mwingine alimsaidia mtuhumiwa kufungua shauri moja kwenye mahakama mbili tofauti kwa lengo la kuwa na hukumu mbili tofauti kwenye kosa moja.

Maadili ya kazi ya utumishi ni sifa ya msingi kwa mtu anayeajiriwa katika ofisi za umma na pale inapobainika kwamba ameyakiuka, anakuwa amepoteza sifa ya kufanya kazi katika ofisi za umma.

Uamuzi uliofanywa na mahakama sio kitu cha ajabu, bali ni utamaduni wa kawaida wa kuwachukulia hatua watumishi wa umma wanaokiuka maadili ya utumishi au kutenda kinyume cha kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Suala la msingi ni kwamba uamuzi huo wa mahakama umefanyika baada ya kufuata taratibu zote ikiwamo kuwa na ushahidi usioacha shaka yoyote.

Tunaipongeza mahakama kwa uamuzi huo, ambao unaonyesha kwamba mhimili hautaki kuwapa nafasi watumishi wasiozingatia maaadili.

Mahakama ni chombo cha kutoa haki, hivyo, inapotokea watumishi wake hususani mahakimu ambao ndio wenye jukumu la kutoa haki wakajihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili, inatia doa na kutoa picha mbaya kwa umma.

Ukweli huo unadhihirishwa na kauli ya Jaji Mkuu Chande kwamba: “Hii ni idadi ndogo ya watendaji wa mahakama, kwa sababu kwa taarifa ya Machi tulikuwa na wafanyakazi 6,406, (hivyo) waliofukuzwa ni asilimia 0.005 tu ya wafanyakazi wa mahakama, ni wachache lakini ni doa.”

Tunashauri kuwa hatua hizo ziwe endelevu kwa kuwa zitasaidia kuwaondoa watumishi wengi wanaokiuka maadili na kuutia doa.

Tunashauri hivyo kwa sababu ripoti nyingi za utafiti zimekuwa zikiitaja mahakama kuwa ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo zinatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wake.
Mahakama inapaswa kuwa mfano katika suala zima la maadili ya utumishi.

Uamuzi uliofanywa na mahakama unapaswa kuwa changamoto kwa taasisi zingine za umma katika kumuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma.

Kuwachunguza watumishi wote wa umma na kuwaondoa watakaobainika kukiuka maadili ya utumishi, kutasaidia kubakiza watumishi wenye nidhamu, waaminifu, weledi, waadilifu na wachapakazi.

Vilevile hatua hiyo itasaidia serikali na taasisi zake kutoa huduma nzuri kwa wateja wake na umma kwa ujumla kwa tija na ufanisi.

Habari Kubwa