Hatua za kushusha bei ya  mafuta zinahitaji usimamizi

11May 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hatua za kushusha bei ya  mafuta zinahitaji usimamizi

SERIKALI jana ilitangaza hatua mbalimbali za kupunguza bei za mafuta ifikapo Juni Mosi, mwaka huu, lengo likiwa kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.

Kupanda kwa bei za mafuta kulitangazwa wiki iliyopita hatua ambayo imesababisha bidhaa mbalimbali kupanda gharama pamoja na usafiri wa vyombo vya usafiri, sababu kubwa ya kupanda kwa bei hizo ni vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine. 

Kutokana na kupanda huko kwa bei, Bunge liliingilia kati na kuitaka serikali kupitia Waziri wa Nishati, January Makamba, kupeleka majibu ya namna ilivyojipanga kupunguza ukali wa bei ya mafuta kwa wananchi na hatimaye jana aliwasilisha taarifa hiyo. 

Waziri Makamba aliweka bayana kwamba serikali imesikia kilio cha wananchi na kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kutoa ruzuku ya Sh. bilioni 100, ilifikapo tarehe iliyoahidiwa na bidhaa hiyo iwe imeshuka bei. Nafuu nyingine, kwa mujibu wa Makamba ni kupata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) utakaopatika mwaka ujao wa fedha.

Hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuruhusu wenye uwezo wa kuagiza na kuingiza  mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo huku serikali ikitangaza kupunguza matumizi ya serikali kwa muda uliobaki wa mwaka wa fedha 2021/22.Kwa uamuzi huo, serikali inastahili pongezi kwa kutekeleza jambo hilo na kuonyesha kwa vitendo kuwa ni sikivu katika kutatua kero za wananchi wake. Ni imani kwamba  uamuzi huo ukisimamiwa vyema, utaleta nafuu kwa wananchi ambao wameingia kwenye ugumu wa maisha kutokana na kupaa kwa bidhaa na huduma.Hata hivyo, ni vyema serikali ikaliangalia vyema suala la kuruhusu wafanyabiashara binafsi kuagiza mafuta nje ya nchi kwamba isigeuke kuwa adhabu baadaye kwamba wanaweza kuungana na kutengeneza uhaba wa bidhaa hiyo.Tunatambua kwa sasa tunatawaliwa na soko huria kwamba kuna ushindani unaoamua soko ya bidhaa husika, lakini lazima kuwa na mifumo ya kusimamia ili isifike wakati ukatengenezwa uhaba wa bidhaa hiyo ili kupandisha bei.Ni muhimu kufanya utafiti wa kina na kujifunza kutoka kwa nchi zinazofanya hivyo, kujua changamoto na fursa zilizopo ili nchi isiingie kwenye matatizo makubwa yatakayoendeleza ugumu wa maisha kuliko hali ilivyo sasa.Pia kwenye kupunguza matumizi wananchi wanapenda kuona kwa uhalisia, kwa kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mfumuko wa shughuli zilizorejesha utengenezaji wa sare mbalimbali na vifaa ambavyo kimsingi ukifuatilia ni fedha nyingine imetumika.Tunatambua ni muhimu kuwa na sare, kutengeneza kalenda na vitabu, lakini tujiulize kwa hali ya uchumi wa nchi yetu ni muhimu kufanya hivyo sasa? Kwanini fedha hizo zisisaidie kuweka ruzuku kukabili changamoto iliyopo.Tunaamini mwananchi anapopitia hali ngumu ya maisha kwasababu ya kupaa kwa mafuta, anatamani kusikia lugha ya kupooza makali kutoka kwa serikali, na ndicho kilichofanyika, lakini sasa ni muhimu kudhibiti wizi wa fedha za umma, ili zielekezwe kwenye utekelezaji wa majukumu muhimu.

Habari Kubwa