Hatua zaidi zichukuliwe kuepuka ajali barabarani

03Sep 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Hatua zaidi zichukuliwe kuepuka ajali barabarani

JESHI la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama barabarani limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti wingi wa ajali barabarani ambazo huacha athari kubwa ikiwamo vifo na ulemavu.

Kampeni mbalimbali za kuelimisha umma zimeendelea kuchukuliwa kila uchao. Aidha, matumizi ya vifaa vya kupima mwendokasi wa magari barabarani maarufu kama ‘tochi’ yameendelea kuongezeka na hivyo, kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya ajali hizo.

Kadhalika, yapo pia matumizi ya vipima ulevi , ukaguzi wa mara kwa mara wa uimara wa magari na ukaguzi wa leseni za madereva ili kubaini weledi wao katika kazi hiyo.

Hakika, zipo jitihda nyingi zinafanywa na hivyo, pongezi zinapaswa kuliendea jeshi hilo.

Jambo hilo ni muhimu kuungwa mkono kutokana na ukweli kuwa madhara ya ajali ni makubwa katika jamii. Watu wasio na hatia hupoteza maisha yao, wengine kuwa walemavu na mali za thamani kubwa huharibika.

Hata hivyo, taarifa kuhusiana na ajali iliyotokea juzi kwenye barabara ya Morogoro, katika eneo la Ujenzi, Kibaha mkoani Pwani, zinaashiria kuwa bado kuna madereva wasiotaka kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani na hivyo, hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kuwadhibiti.

Taarifa kuhusiana na ajali hiyo, zilieleza kuwa mtu mmoja alifariki dunia, mwingine alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa hoi taabani na majeruhi wengine kadhaa walilazwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha.

Waathirika wa ajali hiyo, wote walikuwamo katika basi la abiria lililokuwa likielekea jijini Dar es Salaam na kugongwa na lori aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa kwa kasi pasi na tahadhari na dereva aliyebainika baadaye kuwa alikuwa amelewa chakari.

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, dereva huyo wa lori aliyesababisha ajali, alikutwa pia akiwa na chupa za pombe na misokoto mitano ya bangi.

Aidha, wakati huo alikutwa pia akiwa na kiwango chga ulevi kinachofikia kipimo cha 105, ambacho ni cha juu zaidi kwa kutambua kuwa kiwango cha mwisho ni cha kipimo cha 20.

Hakika, hii ni ajali inayosikitisha. Inaumiza kwa sababu aliyekufa na wale waliojeruhiwa wakiwamo watoto wa shule ya msingi, hawana hatia yoyote. Uzembe wa mtu mmoja aliyeamua kukiuka sheria kwa kuendesha gari huku akiwa amelewa chakari ndiyo chanzo cha msiba huo.

Ni katikam mazingira kama hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa sasa kuna kila sababu kwa jeshi la polisi na jamii yote kwa ujumla kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya madereva wa aina hiyo. Kwamba, wafikishwe kwenye mkono wa sheria na adhabu kali dhidi yao ichukuliwe ili kutoa funzo kwa wengine.

Aidha, licha ya kutambua na kupongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa katika siku za hivi karibuni na jeshi la polisi na wadau wengine wa usalama, sisi tunaona kuwa bado kuna haja ya kuongeza kasi zaidi ya kampeni zisizokoma za kutoa elimu ya usalama barabarani.

Kwa mfano, kama uelewa ungekuwa wa kutosha kwa kila mmoja na siyo kusubiri polisi wa usalama barabarani peke yake, ni wazi kwamba dereva mlevi aliyesababisha ajali ya Kibaha asingefika mbali kutoka huko alikotoka. Walio karibu naye wasingemuacha apande gari na kushika usukani kwa nia ya kuliendesha.

Na walioliona gari hilo likikatiza kwa kasi ya ajabu kwenye barabara ya Morogoro, kamwe wasingemuacha afanye hivyo kabla ya kutoa taarifa polisi ili atiwe mbaroni kabla ya kusababisha maafa.

Shime, elimu ya usalama barabarani iendelee kutolewa ili kudhibiti matukio ya ajali zinazoepukika.

Habari Kubwa