Hatua zichukuliwe kudhibiti mbinu mpya pombe viroba

17Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua zichukuliwe kudhibiti mbinu mpya pombe viroba

KWA siku mbili mfululizo kuanzia jana, Nipashe tunachapisha ripoti maalum kuhusu mbinu mpya za kificho zilizobuniwa na wafanyabiashara kuuza pombe kali zisizokidhi viwango mijini, hasa jijini Dar es Salaam.

Ripoti hiyo ambayo ni matokeo ya uchunguzi wa miezi minne jijini Dar es Salaam, inabainisha kuwa wapigadebe, madereva, makondakta, wamebeba mizigo, waendesha maguta na wafanyabiashara ndogondogo, maarufu machinga, ndiyo wateja wakubwa wa pombe hizo.

Ndani ya mtazamo huo, kuna kuibuliwa kwa mbinu mpya za udanganyifu zinazofanywa na wafanyabiashara, pia wachuuzi wa viwanyaji hivyo haramu kuhakikisha walichokuwa wakifanya awali kinaendelea kuwapo, licha ya amri kali ya serikali inayotimua mwaka wa tatu sasa.

Kimsingi, serikali ilipiga marufuku biashara ya kuuza pombe kali kwenye mifuko midogo ya plastiki, maarufu viroba kuanzia Machi Mosi, 2017.

Uchunguzi wetu, hasa jijini Dar es Salaam, umebaini kupamba moto biashara ya vinywaji hivyo haramu, mbinu ya mlango wa pili unaotumiwa sasa ni namna ya ufanyikaji wake ni kificho kipya kinachoendeshwa kupitia ushirikiano wa aina yake kati ya wauzaji na wateja.

Ni nyendo zinazokinzana na agizo zito la marufuku lililotolewa na Mtendaji Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye aliweka bayana kwa watakaothubutu kukiuka, watakutana na mkono wa dola kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Matabibu ambao ndiyo wanaohudumia waathirika wa vinywaji hivyo, wanaungana na Waziri Mkuu wakiwa na lao. Daktari Bingwa wa Macho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Catherine Makunja, anadokeza walakini wa jumla katika ubora wa vilevi hivyo, usafi wa chupa na glasi zinazotumika, hata usindikaji wake, huku mnywaji akikaribisha kuugua presha ya macho.

Dk. Onesmo Kisanga, bingwa wa tiba ya figo - MNH, pia anavihusisha vilevi hivyo na chanzo cha kuugua figo, ambayo huwa haina mwisho mzuri kwa afya ya binadamu, ikiwamo kifo kama ilivyo kwa presha ya macho.

Kwa kuzingatia mtazamo huo, Nipashe tunaona mamlaka husika za serikali, kila moja kwa nafasi yake, kuchukua hatua stahiki kuzuia biashara hiyo haramu ili kuokoa afya ya wananchi.

Wapigadebe, madereva, makondakta, wamebeba mizigo, waendesha maguta na wafanyabiashara ndogondogo waliotajwa kuzama kwenye utumiaji wa vilevi hivyo ni kundi la vijana ambao ni nguvukazi ya taifa la leo na kesho.

Ni katika uzito huo, Nipashe tunaona mamlaka husika za serikali zinapaswa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na wafanyabiashara na wachuuzi wa pombe hizo wenye nia ya kujipatia fedha kwa kuzalisha au kuuza bidhaa zisizokidhi viwango pasi na kujali madhara yake kwa afya za walaji.

Kuna madhara mengi na makubwa yanayoweza kutokea na kuwaathiri watumiaji wa bidhaa hizo, vikiwamo vifo. Hivyo ni matarajio yetu kuona hatua hizo zikianza kuchukuliwa na mamlaka zetu ili kuwabaini wote wanaojihusisha na mchezo huo mchafu.

Ni wakati mwafaka sasa wahusika hususani Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuanzisha msako wa kuwabaini watu hao kisha kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.

Habari Kubwa