Hatua zichukuliwe magonjwa yasiyoambukiza yanaangamiza

24Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua zichukuliwe magonjwa yasiyoambukiza yanaangamiza

NOVEMBA 3 mpaka 6, mwaka huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kupitia Taasisi ya Mpango wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), inaadhimisha Wiki ya Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza, jijini Arusha.

Lengo la maadhimisho hayo ni kuwakumbusha na kuwahamasisha Watanzania umuhimu wa kuangalia afya zao mara kwa mara ili kujiepusha na athari za magonjwa hayo.

Magonjwa yasiyoambukiza ni yale yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa mfano magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari, kuoza meno, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama selimundu.

Serikali inatumia gharama kubwa katika bajeti yake kutibu magonjwa yasiyoambukiza na kwa mwaka 1991 ilionyesha kuwa asilimia tisa ya bajeti ilitibu wagonjwa wa kisukari.

Kwa mujibu wa wataalamu wa TANCDA, magonjwa haya yanaongezeka kwa kasi na kuwaathiri hata watu wenye umri mdogo wakiwamo watoto.

Mwaka 2016, watu milioni 42 (sawa na asilimia 71 ya vifo vyote) walifariki duniani kutokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Asilimia 75 ya vifo vyote vinavyohusu watu wenye miaka 30 -70 husababishwa na magonjwa hayo.

Sababu zinazoelezwa za kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwamo kutofanya mazoezi, kukaa ofisini, darasani kwa muda mrefu, kuangalia runinga, kutumia lifti kupanda majengo ya ghorofa, kupanda magari na kutoshiriki michezo.

Sababu nyingine ya kuongezeka kwa magonjwa hayo ni ulaji usiofaa, kwa mfano kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, kula sukari, mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili, kutokula mboga na matunda kiasi cha kutosha, kula nafaka zilizokobolewa na kunywa juisi badala ya matunda yenyewe.

Wataalamu hao wanasema pia matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya yanachangia magonjwa yasiyoambukiza, vile vile msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha.

Ili kuepukana na magonjwa hayo inashauriwa kufanya mazoezi na kila mlo uwe na makundi yote matano ya vyakula ambayo (a) ni nafaka, mizizi, ndizi mbichi za kupika, (b) matunda, (c) mboga, (d) jamii ya mikunde na asili ya wanyama na (e) mafuta.

Chakula mchanganyiko humwezesha mtu kupata virutubishi vyote vinavyohitajika mwilini, ikiwamo wanga ambao husaidia kuupa mwili nguvu na joto. Vyakula vya protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa.

Wataalamu wanashauri kuwa mwili unahitaji nguvu kila dakika, hivyo ni vizuri kula kila njaa inapouma. Milo mitatu kwa siku, pamoja na asusa moja asubuhi na nyingine jioni. Kifungua kinywa ni muhimu kila asubuhi kwa kuwa mtu anapoamka akiba ya sukari mwilini huwa ndogo baada ya muda mrefu bila chakula.

Katika utafiti uliofanywa mwaka 2012 nchini ulioshirikisha watu wenye umri wa miaka 25 na kuendelea, kwa kila watu 14 waliokutwa na shinikizo la juu la damu, ni mmoja pekee kati yao ndiye aliyekuwa amegunduliwa tayari.