Haya yafanyiwe kazi TRA kuongeza mapato

09Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Haya yafanyiwe kazi TRA kuongeza mapato

APRILI 6, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, alirudia agizo lake kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuacha kuwanyanyasa wafanyabiashara na wawekezaji, jambo ambalo limefukuza wengi kwenda kuwekeza katika nchi nyingine duniani.

Aidha, alionyesha kusikitishwa na ubabe, uporaji unaofanywa na maofisa hao ambao walikuwa kwenye kikosi maalum, ambacho kiligeuka kufanya dhuluma kwa wafanyabiashara.

Rais Samia alisema zaidi kwamba hatahitaji kodi ya dhuluma na kama watakusanya kodi ya dhuluma, ni heri wasikusanye kwa kuwa siku zote dhuluma haina safari ndefu, na siyo haki mbele ya Mungu.

Vitabu vitakatifu vimesema ya Kaisari (dola) mpe Kaisari na ya Mungu mpe Mungu, yaani inatambulika kodi na ada mbalimbali za kisheria ni kwa wahusika, huku Mungu yake ni fungu la kumi, zaka, sadaka ya malimbuko, sadaka ya amani na nyinginezo ambazo zimetajwa.

Kilio cha wafanyabiashara kimekuwa kikubwa kwa kuwa ilifikia mahali wengi kuonekana ni wezi, wapigaji na kodi za nyuma kutumika kama fimbo ya kuwachapa, kiasi kwamba wengi wamefilisika.

Athari za yaliyokuwa yanafanyika ni wafanyabiashara kuondoa fedha benki na kuzificha nyumbani, kwa kuwa kila walivyoonekana na kiasi fulani benki zilichukuliwa na kushindwa kujiendesha, jambo ambalo ni baya.

Wafanyabiashara hawa wenye uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini walifunga shughuli zao, hivyo kusababisha Watanzania wengi walioajiriwa kwenye sekta binafsi kupoteza ajira na mzunguko wa fedha kupungua.

Rais Samia ameliona tatizo na kutoa maelekezo ya kulishughulikia ili kurudisha fedha kwenye mzunguko na kujenga imani kwa jumuiya ya wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla.

Hakuna ubishi kuwa kampuni na biashara nyingi zimefungwa, na siyo kwa kupenda bali mazingira yalikuwa yenye kuumiza na kutishiwa kubambikiwa kesi za uhujumu uchumi na hata maisha yao.

Tunaamini kwa mabadiliko ya uongozi ambayo Kamishana Mkuu wa sasa, Alphayo Kidata, ambaye alishapita TRA, kutakuwa na nuru njema na sasa watu watafanya biashara na kulipa kodi zote muhimu kwa mujibu wa sheria.

Lakini tunakifiri haitoshi kushughulikiwa suala hili bila kwenda kwenye mzizi wa tatizo, kwa kuangalia upya sheria za kodi na uanzishaji biashara, ambazo zimelalamikiwa kwa muda mrefu na hata Ripoti ya Hali ya kufanya Bishara Tanzania inayotolewa na Benki ya Dunia (WB), imeainisha vikwazo mbalimbali.

Kuvunja kikosi kazi na kukemea ubabe, unyang’anyi na dhuluma nyingine haitoshi, maana ni sawa na kutibu kidonda kwa juu wakati ndani bado hakijapona, bali tunashauri kinachotakiwa kufanyika ni kupitia upya sheria mbalimbali ambazo ni tatizo kubwa.

Ukuaji wa biashara utaongeza ajira kwa wingi na kupunguza wategemezi na wasio na ajira, ambao wangeingia kwenye wizi na shughuli nyingine zisizo halali.

Kiwango cha ajira kimeendelea kupungua kila siku, na hao hao wanaotarajiwa kulipa kodi walibanwa kiasi cha kufilisika, hali ambayo ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa kwa muda mfupi lakini siyo endelevu.

Tunampongeza rais kwa kuliona hilo, lakini bado tunamuomba jicho lake limulike kila mahali na sasa tuone ujenzi wa sekta binafsi imara ambayo itakuwa na nguvu ya kuajiri mamia ya wananchi ambao sasa wako mtaani licha ya kuwa na utaalamu mwingi.

Serikali yoyote inayotaka kufanikiwa katika kukusanya kodi huimarisha sekta binafsi kwa kujenga mazingira wezeshi na siyo kuiua, kwa kuwa hakuna ubishi kuwa serikali haiwezi kuajiri wala kutengeneza ajira nyingi.

Itakuwa ni hujuma kama viongozi wa serikali watakuwa na fikra kuwa serikali inaweza kufanyakazi yenyewe kwa yenyewe na haihitaji sekta binafsi, jambo ambalo huko nyuma lilishindikana kwa kuwa mashirika na viwanda vingi vya umma kama Kiwanda cha General Trye vilikufa, lakini usimamizi na uendeshaji wa sekta binafsi ulifufua na kuleta tumaini la maisha.

Habari Kubwa