HESLB hongera kwa kujiboresha

06Jun 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
HESLB hongera kwa kujiboresha

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetoa mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 unaotaja sifa, vigezo na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Hatua hii kwa hakika ni ya kupongeza.  Kwa kuwa mwongozo pia umeandaliwa katika lugha za Kiingereza na Kiswahili na kuuweka katika tovuti ya HESLB ambayo ni www.heslb.go.tz inalenga kuwawezesha waombaji au wazazi ambapo wengine hawajui lugha ya Kiingereza sasa wataupata kwa urahisi na kujisomea hivyo kupunguza au kuondoa kabisa usumbufu wa kulazimika kufika kwenye ofisi hizo.

 

Pamoja na mwongozo huo HESLB wameandaa kitabu chenye maswali na majibu yanayoelekeza namna ya kuomba mkopo kwa lugha ya kiswahili ambacho pia kinapatikana kwenye tovuti yao, hivyo tunaamini kwamba idadi ya waliokosa mikopo kutokana na kukosea kujaza fomu kwa kukosa mwongozo itapungua sasa.

 

Wameweka wazi nyaraka muhimu zinazotakiwa ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa ambavyo vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA). Aidha, kwa waombaji mikopo ambao wazazi wao wamefariki dunia, watatakiwa kuwa na nakala za vyeti vya vifo ambavyo vimethibitishwa na RITA au ZCSRA.

 

Mambo hayo yatapunguza usumbufu kwa waombaji wa mikopo hiyo kwa kuwa watapata nafasi ya kujiandaa kabla ya kuanza kujaza fomu za kuiomba.

 

Tunawapongeza viongozi wa HESLB chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru

kwa usikivu kwani wamebainisha wazi kuwa baadhi ya maboresho wameyafanya baada ya kupokea maoni ya wadau.

 

Maboresho hayo ni pamoja na kuongeza umri wa waombaji mikopo kutoka miaka 33 hadi 35 na pia mwaka huu wameahidi kuwa watapokea maombi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano iliyopita badala ya miaka mitatu ilivyokuwa awali.

 

Hii ni habari njema kwa wadau wa elimu na wazazi kwamba mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali kupitia HESLB imepanga kutoa mikopo na ruzuku ya elimu ya juu yenye thamani ya Sh. bilioni 450 kwa jumla ya wanafunzi 128,285.

 

Kati ya hao, wanafunzi 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza. Mwaka huu 2018/2019, unaoelekea mwisho jumla ya Sh. bilinioni 427.5 bilioni zilitolewa kwa jumla ya wanafunzi 123,000.

 

Hatua hii ilitakuwa na manufaa makubwa kwa jamii yetu kwani kuongezwa kwa idadi ya wanufaika wa mikopo na kiwango cha fedha za mkopo ni wazi kwamba itaongeza idadi ya wasomi nchini.

 

Pia kulikuwa na malalamiko makubwa kuhusu kukosa mikopo kwa baadhi ya wanafunzi walioonekana kusoma kwenye shule binafsi za gharama, hivyo kuonekana kuwa wazazi au walezi wao wanauwezo wa kuwalipia hata ada ya elimu ya juu nalo limepatiwa ufumbuzi kwa namna yake.

 

HESLB imewataka wanafunzi waliofadhiliwa na taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari au stashahada, kuwa na barua kutoka katika taasisi hizo zinazoonyesha jinsi walivyokuwa wanafadhiliwa kwa kuwa miongoni mwao wapo yatima au waliotoka kwenye familia zenye kipato duni hivyo walinufaika kusoma kwenye shule hizo kwa fadhila.

 

Jambo hili linatia moyo kwa kuwa miaka kadhaa iliyopita kuna yatima na watoto wa masikini walikwama kuendelea elimu ya juu kutokana na kwamba mashirika au taasisi zilizowafadhili hazikuweka utaratibu wa kugharamia masomo yao zaidi ya yale ya sekondari au mafunzo kwenye vyuo kwa kiwango cha stashahada.

Habari Kubwa