HESLB iharakishe rufani wahitaji

14Nov 2017
Mhariri
Nipashe
HESLB iharakishe rufani wahitaji

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) juzi ilitangaza orodha nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupata mikopo, ikiwa ni awamu ya nne.

Kutolewa kwa orodha hiyo mpya kunafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa na HESLB kufikia 31,353.

Ikumbukwe kuwa katika awamu ya kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, na kufuatiwa na 11,481 wa awamu ya pili na kisha 7,901 katika awamu ya tatu, kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Tunaipongeza HESLB, Nipashe, kwa kukamilisha idadi hiyo ya wanafunzi na kwa kuhakikisha orodha kamili ya wanafunzi waliopangiwa mikopo imetumwa kwa vyuo husika ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo, lakini pia orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi ya www.heslb.go.tz.

HESLB isingeweza kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 31,353 wa mwaka wa kwanza, Nipashe tunafahamu kama si kuwezeshwa kiasi cha Sh. bilioni 427.54 na Serikali.

Tunafahamu Nipashe kuwa kiasi hicho kimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa Sh. bilioni 147.06 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/2018.

Lakini katikati ya pongezi zetu, Nipashe, kwa HESLB tunapenda pia kuchukua fursa hii kuishauri bodi kuona uwezekano wa kuharakisha zaidi mchakato wa rufaa kwa wanafunzi stahiki walioomba lakini majina yao yamekosekana katika orodha nne hadi sasa.

Taarifa ya HESLB imesema bodi hiyo imetangaza kufungua dirisha la rufani kuanzia jana hadi Jumapili ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufani kupitia vyuo walivyopata udahili.

Aidha, HESLB imesema lengo lake ni kuhakikisha inatangaza majina yote ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufani zao ifikapo au kabla ya Novemba 30.

Ingawa Novemba 30 ni wiki mbili na nusu zijazo, ni mbali, Nipashe tunaona, kwa wanafunzi ambao wanasubiri kuanza masomo ambayo yalianza tangu Oktoba 30 kwa kuwa watajikuta wakiwa nyuma ya mtaala kwa zaidi ya mwezi mzima wakati HESLB ikitoa matokeo hayo.

Tuchukue fursa hii, basi, Nipashe, kuishauri HESLB kutoa majibu ya rufani hizi kila siku kwa kila ambaye atakuwa ameshinda rufani yake ili kuokoa japo wachache kati ya wanafunzi hao na kupoteza muda mwingi nje ya madarasa wakati wenzao wakiendelea na kozi kwa mwezi mmoja sasa.

Na kwa sababu HESLB haitaweza kuhakarikisha mchakato huo bila wakuu wa vyuo kutimiza wajibu wao, tunawaomba nao, pia, kutimiza jukumu hilo kwa wakati kama ambavyo bodi imeomba.

Uongozi wa vyuo vyote upokee maombi ya rufani za wanafuzi na kuwasilisha HESLB kila mwisho wa siku ya kazi ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufani zao kila siku pia, Nipashe tunaomba.