Hifadhi Ruaha sasa  ifungue fursa zaidi

01Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Hifadhi Ruaha sasa  ifungue fursa zaidi

TANZANIA imeendelea kupaa kimataifa katika sekta ya utalii, baada ya mtandao wa National Geographic kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kuwa sehemu muhimu ya kutembelewa na watalii mwaka 2018

Hifadhi ya Ruaha ni ya kwanza kwa ukubwa nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na imetambaa katika vijiji 64 vya wilaya za Iringa na Mufindi katika mkoa wa Mbeya, Chamwino (Dodoma), Wangiing’ombe (Njombe), Mbarali na Chunya (Mbeya).

Kwa mujibu wa mtandao huo, Ruaha ni kivutio bora kutembelewa duniani kwa mwaka 2018 kwa kuwa ni hifadhi yenye simba wengi zaidi.

Mtandao huo unasema ndiyo hifadhi unayoweza kuona simba wakiwa kwenye makundi ya idadi ya (wanyama) 10 hadi 30 au zaidi sambamba na kuona uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa urahisi zaidi na kwambaidadi ya simba ni kubwa.

Kutajwa kwa Ruaha kuwa sehemu muhimu ya kutembelewa na watalii kwa mwaka 2018, ni habari njema kwa wadau wa utalii, serikali na Watanzania wote kwa kuwa itaiwezesha hifadhi hiyo kuliongezea mapato Taifa letu kutokana na uwezekano wa kuongezeka idadi ya watalii watakaoingia nchini kuona wanyamapori hususan simba. 

Ni matarajio yetu hifadhi ya Ruaha itaitumia fursa hiyo kufanya maandalizi ya kutosha hususan kuweka mazingira mazuri ya kupokea watalii wengi.

Mazingira mazuri ni pamoja na kuboresha huduma muhimu kama miundombinu ya barabara na uwanja wa kisasa wa ndege, hoteli, ulinzi wa uhakika pamoja na huduma zingine ambazo watalii wanaweza kuzipata nje ya hifadhi. 

Tunapaswa kuichukulia fursa hiyo kwa Ruaha kuwa ni changamoto siyo kwa hifadhi hiyo pekee bali kwa serikali, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na wadau wote wa utalii, lengo likiwa ni kupata idadi zaidi ya watalii.

Serikali imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tatu kwa mwaka, hivyo lengo hilo linaweza kufikiwa kama hifadhi zetu na vivutio vingine vinavyovutia zaidi watalii vitatangazwa zaidi na kuboreshwa.

Bado tunayo safari ndefu ya kufikia lengo la watalii milioni tatu kwa mwaka. Kwa mujibu wa Mtango Mtahiko, Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Tanapa, mwaka 2015 hadi Septemba mwaka huu, 2016 watalii 982,340 walitembelea hifadhi za Taifa.Kwa hiyo changamoto iliyopo ni kuendelea kuboresha hifadhi zote za taifa ambazo ni 16, mapori ya akiba 42 na mapori tengefu 28 ili watalii wavutike na kuja kutembelea vivutio vilivyopo na nchi kuongeza mapato kupitia sekta ya utalii.

Jambo la kutia moyo na matumaini ni kauli ya Mhifadhi Mkuu wa Ruaha, Dk. Christopher Timbuka, ambaye aliliambia gazeti hili juzi baada ya mtandao wa National Geographic kuitaja hifadhi yake kuwa matarajio yao ni kuongezeka wa idadi ya wageni.

Alisema wamejipanga kupokea watalii wengi na kuwahimiza waliopewa maeneo ya uwekezaji ya ujenzi wa hoteli za kitalii kuharakisha ili ifikapo mwaka 2018 wakamilishe.

Anasema kwa sasa wanapokea wastani wa watalii 25,000 kwa mwaka na kwamba wana vitanda 377 hifadhini.

Ili kukabiliana na ungezeko la idadi ya watalii mwakani, ipo haja pia ya kuongeza idadi ya vitanda ili ikidhi mahitaji ya ongezeko hilo la watalii.

Tunaishauri Tanapa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wanafuatilia na kuratibu kwa ukaribu ili watalii watakaoingia mwakani na kutembelea Ruaha wapate huduma nzuri na nchi yetu inufaike na ujio wao.

Ieleweke kuwa hatuwezi kunufaika na mapato ya utalii kama hakutakuwa na uwekezaji wa fedha katika sekta hiyo. 

Habari Kubwa