Hili linawahusu nyie viongozi halmashauri

29Aug 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hili linawahusu nyie viongozi halmashauri

KATIKA gazeti letu la jana, tuliandika habari yenye ujumbe wa Waziri kumpa Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, jukumu la kuwacharaza viboko watumishi wenye utendaji wa mwendo wa konokono.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ndiye anayetoa maelekezo hayo, kwenye kutia saini ujenzi na uwekezaji wa vitega uchumi jijini Dodoma.

Waziri anachosema kinamaanisha kuwachagiza watumishi wa halmashauri kufanyakazi kwa wakati, bidii  na kwa ufanisi  badala ya kutoa  visingizio kibao, kuchelewesha kazi na hata wakati mwingine kuzikwamisha.

Waziri anachosema ni kweli kwa sababu miradi mingi katika halmashauri haifanyiki kikamilifu na kwa wakati. Kinachoweza kutumiwa ni kutoa maelezo kama meya hajasaini, madiwani hawajaidhinisha au yanasubiriwa maoni ya mtunza hazina wa halmashauri.

Pamoja na Waziri Jafo kutoa maagizo ya ufuatiliaji huo, ni wakati wa kuwa na mikakati na programu za kuuchunguza utendaji kazi wa viongozi wanafanyaje kazi?

Tunajiuliza hivi inapotokea Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi wa ujenzi hospitali ya wilaya na serikali imetoa fedha, lakini kazi haifanyiki ni nani anayekwamisha? Ni Mkurugenzi wa Halmashauri anayezuia fedha, ni meya na madiwani, mtunza hazina, je, ni mkandarasa asiye na uwezo? Miradi inapokwama ni wazi kuwa wapo maofisa wa halmashauri wasiotimiza wajibu.

Iwapo serikali imeshatoa fedha za ujenzi wa hospitali ya wilaya, ardhi imeandaliwa? Ofisa ardhi amepima kiwanja? Wahandisi wa ujenzi wamekadiria gharama? Wataalamu wa zabuni wameziandaa na kuzitangaza? Kama yote yamefanyika mkwamo uko wapi?

Tunaona kuwa hicho ndicho Waziri Jafo anachotaka kifanyike kila mmoja atimize wajibu wake na kama hatimizi ni nani wa kumbana? Katika utaratibu huo wa Jafo wa kutandika watendaji viboko suala la uwajibikaji ni muhimu.

Tunampongeza Waziri Jafo kwa sababu imekuwa ni mazoea kazi hazifanyiki mpaka wakati wa ziara za Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu au pengine Waziri ndipo hoja zinapoibuliwa kuwa barabara, zahanati na shule hazijakamilika?

Tunajiuliza inakuwaje barabara isimalizike hadi ujio wa Rais kijijini au mkoani hapo? Watu wanapotoa malalamiko kwa kiongozi ndipo kazi inapokamilika? Siku zote hizo watu wanakuwa wapi wasifanye kazi hadi kufokewa na viongozi?  

Maelekezo hayo ya Waziri Jafo, yafanyiwe kazi  na inapotokea changamoto kama hizo  viboko vitembee kwa maana ya ufuatiliaje ifahamike uzembe ulikuwa wapi na mhusika anacharazwa bakora ili ionekane tatizo la uwajibikaji lilianzia wapi na uwajibikaji ulikwamia  wapi ili sera na sharia zitumike  kwenye uwajibikaji.

Pamoja na kutotekelezwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo, suala jingine ambalo linahitaji watu kucharazwa viboko ni hili la kazi kwa ‘mazoea’ mfano bomba zinavuja iwe vyooni, uwanjani au kwenye matangi ya kuhifadhi maji.

Katika mazingira kama hayo  hakuna wa kuzikarabati na kila siku maji yanapotea bila viongozi wa halmashauri kuwajibika wala kuwajibishana.

Katika mazingira kama hayo ofisi nyingi za umma taa za umeme zinapoungua hakuna wakiziangalia, vitasa vikivunjika na masinki ya vyoo yakiharibika  hakuna anayewajibika moja kushughulikia matatizo hayo.

Tunaona kuwa kupuuza huko mambo wanayoamini kuwa ni madogo kama bomba zinazovuja na viti vilivyovunjika ofisini, kunaendeleza mlolongo wa uzembe kwenye miradi mikubwa kama barabara, ujenzi wa vitega uchumi, ofisi za umma,  hospitali na visima au miradi ya maji.

Kwa hiyo utaratibu wa kucharaza viboko kwa maana ya kufuatilia na kubaini viongozi viraka ni muhimu ili kujua nani anayekwamisha maendeleo.

Habari Kubwa