Homa Dengue bado tishio, tusibweteke wagonjwa kupungua

05Jul 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Homa Dengue bado tishio, tusibweteke wagonjwa kupungua

MARA nyingi kuna tabia ya jamii kubweteka na kuacha kuchukua tahadhari pale tatizo linalowakabili linapopungua au kwisha kabisa.

Hali hiyo ya jamii kubweteka imekuwa ikitokea kwa changamoto mbalimbali, yakiwamo magonjwa. Kwa miezi kadhaa mwaka huu, uliibuka ugonjwa wa homa ya Dengue katika mikoa mbalimbali nchini.

 

Ugonjwa huo umesababisha athari kubwa kwa familia kadhaa, vikiwamo vifo, hali iliyoifanya serikali kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba hayatokei madhara zaidi.

 

Miongoni mwa hatua hizo ni kutoa elimu kwa umma kuhusiana na chanzo cha homa ya Dengue, hatua za kuchukua hususan kuwahi katika vituo vya huduma za afya kwenda kupima pamoja na kutengwa kwa vituo rasmi vya huduma kwa ajili hiyo.

 

Elimu kwa umma kuhusiana na tahadhari ya kuchukua pia imekuwa ikiendana na hatua za serikali za kupulizia dawa katika maeneo ya makazi hususan yenye mazalia ya mbu. Kadhalika, serikali imewawekea mazingira mazuri wananchi ya kupima homa hiyo bila malipo.

 

Kimsingi, tunathubutu kusema kuwa ugonjwa huo umekuwa janga kubwa kwa Watanzania, kutokana na familia kadhaa kupoteza wapendwa wao.

 

Katika hali inayotoa matumaini, serikali imesema kuwa sasa kuna ahueni kutokana na kupungua kwa wagonjwa wanaougua Dengue.

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ndiye aliyesema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa anawaongoza wakazi Manispaa ya Ilala kupulizia dawa ya kuua mazalia ya mbu aina ya Dengue, na kueleza kuwa idadi ya waliougua imepungua kutoka watu 2,759 mwezi Mei hadi wagonjwa 790 mwezi uliopita.

 

Hakika hizi ni habari njema na ni za kutia moyo na matumaini kwamba hatua za tahadhari zilizochukuliwa zimewezesha kupunguza makali ya ugonjwa huo.

 

Hilo pia linapaswa kutupa funzo kwamba yanapotokea majanga kama hayo, jamii nzima iwe na mwitikio chanya kwa kuchukua hatua haraka bila kusubiri athari kuwa kubwa zaidi.

 

Jambo la msingi ni jamii kuendelea kuchukua tahadhari na kutochukulia kuwa ugonjwa huo umetokomea kabisa, kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kuukaribisha upya.

 

Wananchi waendelee kusafisha mazingira yao hususan kuhakikisha kwamba mazao ya mbu yahabaribiwa ili mbu aina ya Dengu wasiweze kutaga mayai pamoja na kuhakikisha wanatumua vyandarua.

 

Kwa upande wake, mamlaka zetu ikiwamo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na halmashauri zote ziendelee kutoa elimu na kuhamasisha umma kuchukua hatua za tahadhari.

 

Mamlaka hizo pia ziendelee kusimamia usafi hususan unyunyiziaji dawa za kuua mazalia ya mbu na kuhakikisha kwamba vituo vya kutolea huduma za afya vinaendelea kupiga homa ya Dengue bila malipo, lengo kuwawezesha wananchi wengi kujitokeza kupoma mapema kabla ya kupata madhara makubwa.

Wito wetu kwa wananchi ni kwamba pamoja na kauli ya Waziri Ummy kuwa wagonjwa wa homa ya Dengue wamepungua, lakini wasibweteke, bali tahadhari iwe endelevu.

 

Pamoja na kuchukua tahadhari, tunawashauri pia mtu akisikia dalili za homa hiyo, jambo la kufanya ni kukimbilia katika vituo vya huduma za afya kupima.