Hongera EU kwa kuonyesha njia

24Nov 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hongera EU kwa kuonyesha njia

MWISHONI mwa wiki, mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU), walizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili dhidi ya wanawake yanayoanza Novemba 25 na kufika kilele Desemba 10, mwaka huu.

Mabalozi hao wa nchi za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, Mkuu wa EU nchini, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women) na Taasisi ya Kijamii ya Tanzania Community Initiatives (TACCI).
 
Katika mkutano huo walieleza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, huku kila ubalozi ukiwa na shughuli ya kijamii itakayofanya katika siku zote 16, ambazo moja kwa moja zinaishirikisha jamii na kuwafikia wengi kwa wakati mmoja.
 
Kila balozi na mkuu wa taasisi alieleza mipango ya baadaye na uwajibikaji wa nchi yake pamoja na shughuli walizofanya na watakazofanya, ikiwa ni miradi mbalimbali ambayo ina matokeo chanya kwa wasichana, wanawake na watoto.
 
Mabalozi hao walisema bado hakuna usawa wa kiuchumi hasa katika sekta isiyo rasmi kwa kuwa bado asilimia 81 ya wanaume ndiyo wanapata kipato cha wastani wa Sh. milioni 1.5, huku wanawake asilimia 15 wakipata kipato hicho.
 
Walisema ukatili dhidi ya wanawake ni tatizo la dunia na bado wanawake na wasichana wanapitia unyanyasaji wa kingono, ukatili wa kijinsia, tamaduni kandamizi.
 
Wanasema ili kukabiliana na yote hayo kila mwanajamii ana wajibu wa kukataa na kufikiri kama ni yeye anatendewa yote hayo, na huku kukiwa na kampeni kwenye mitandao ya kijamii kuhamasisha jamii kutokukubaliana na ukatili.
 
Kila ubalozi na taasisi ulitoa hakikisho lake la kuendelea kutoa fedha kwenye miradi ya wanawake, na kuhusisha wanaume ambao ni sehemu ya suluhisho, lengo kuu likiwa ni kupunguza au kumaliza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na kuweka usawa wa kiuchumi.
 
Mabalozi hao wanasema ni lazima wanaume na wavulana kushirikishwa katika kupigania usawa wa jinisia kwa kuwa usawa ni wa manufaa kwa jinsi zote.
 
Mathalani, Ubalozi wa Ufaransa, Ubelgiji na TACCI utakuwa na shughuli za kijamii kama sherehe ya jioni kujadili ukatili wa kujinsia kwa kauli ya ninasimama kupinga ukatili katika mfumo wa taaluma.
 
Hafla hiyo itajumuisha michezo mbalimbali kama ngoma za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuhusu unyanyasaji kingono, nafasi ya wanawake katika ngazi ya maamuzi na ndoa za utotoni.
 
Pia, mabalozi hao watakuwa na burudani ya wazi ikiwa na kauli mbiu ya usiku wa kuwawezesha wanawake kujieleza wenyewe na kupata nafasi mbalimbali katika ngazi zote.
 
Ubalozi wa Uholanzi watakuwa na filamu ya Nigeria kuhusu unyanyasaji wa kingono.
 
Tunazipongeza balozi hizi kwa hatua kubwa ya kushiriki kikamilifu kwa mambo yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja, kwa kuwa miradi hiyo itanufaisha wanawake moja kwa moja.
 
Tunawapongeza kwa kuisaidia jamii ya Watanzania, kwa kuhakikisha mila potofu kama ndoa za utotoni, ukeketaji na ukatili dhidi ya wanawake unakomeshwa.
 
Tunashauri ni vyema fedha za miradi ya kuwasaidia wanawake zinapopelekwa kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali, zitumike vyema na kuwafikia walengwa, ili mabadiliko yanayotarajiwa na wanaotoa fedha za walipakodi wao yafikiwe.
 
Maadhimisho haya yanafanyika wakati ambao kuna ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, kwa kupigwa, kujeruhiwa na kuuawa na waume zao kwa sababu kama za wivu wa mapenzi na nyinginezo ambazo hazina msingi wowote wa kudhuru maisha ya binadamu.

 
 

Habari Kubwa