Hongera Kigwangalla kumalizana tofauti na Katibu Mkuu wake

03Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hongera Kigwangalla kumalizana tofauti na Katibu Mkuu wake

MIONGONI mwa habari zilizotikisa nchi katika kufunga mwaka 2019 na kuingia mwaka 2020 ni juu ya tofauti kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wake, Prof. Adolf Mkenda.

Taarifa ya kutokupatana kwa viongozi hao wakuu wa wizara hiyo, ziliibuliwa na Rais John Magufuli alipofanya ziara Desemba 31, mwaka jana, katika Hifadhi ya Msitu wa Rubondo na kuzungumza na maofisa na askari wanyamapori.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli alisema anasikitishwa na uhusiano mbaya baina ya viongozi hao, ambao kwa kiasi kikubwa ulisababisha baadhi ya shughuli katika wizara kuzorota.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa amekuwa akifuatilia utendaji kazi wa Dk. Kigwangala na Prof. Mkenda ambao umekuwa si wa kuridhisha kutokana na kugombana kwao.

Ugomvi wao huo, alisema umemfanya amwagize Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, awaite na kuwaeleza. Bila kuuma maneno, Rais magufuli alisema wateule wake hao wawili wamekuwa wakigombana kila uchao na kusababisha kazi za wizara kwenda arijojo.

Kutokana na tofauti hizo, aliweka wazi kwamba anawapa siku tano kuanzia Desemba 31, mwaka jana, wamalize tofauti zao, vinginevyo atatumia mamlaka aliyo nayo kutengua uteuzi wao.

Wakati umma ukisubiri kuona tofauti hizo zinazikwa na kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa sekta wanazoziongoza, Dk. Kigwangalla juzi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wamepatana na kuwa kitu kimoja.

Kigwangalla katika ukurasa wake huo, alitanabahisha kuwa baada ya kikao chao na Katibu Mkuu Kiongozi, wamezika tofauti zao na sasa hali ni shwari.

Hizo ni habari njema kwa sababu kupatana kwao ni ishara kuwa wametii maagizo ya Rais kuwa wamalize tofauti zao ili kuiendeleza wizara hiyo ambayo imebeba moja ya sekta nyeti katika kutoa mchango kwenye pato la taifa.

Hatua ya kumaliza tofauti kati ya Dk. Kigwangalla na Prof. Mkenda licha ya kuonyesha ukomavu kutokana na hadhi zao za kielimu, pia kumeonyesha weledi wa hali ya juu na kuleta imani kwamba sasa watafanya kazi kwa ushirikiano na maelewano.

Pamoja na hatua waliyoifikia, kama alivyosema Dk. Kigwangalla, ni vyema ikawa ya kweli badala ya kuwapaka Watanzania kwa mgongo wa chupa au kiutimiza msemo kwamba “funika kombe mwanaharamu apite”. Wawili hao wanajenga nyumba moja, kwa nini kugombea fito?

Mapatano hayo yawe ya dhati na ni imani ya Watanzania kwamba yatakuwa ya kweli na kama yatakuwa ya unafiki, Rais Magufuli, kama alivyosema ana vyombo vya kufuatilia, atabaini kama si ya kweli.

Habari Kubwa