Hongera Rais Magufuli kutwaa uenyekiti CCM

24Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Hongera Rais Magufuli kutwaa uenyekiti CCM

HATIMAYE Rais John Magufuli, alichaguliwa kwa kura zote kushika nafasi ya uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ili kukitumikia chama hicho tawala katika kipindi cha miaka mitano kuanzia jana.

Hatua hiyo iliyotarajiwa, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wa Rais kuwa na kofia mbili ikiwamo ya kuwa kiongozi mkuu wa chama hicho, ilifanikishwa kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa taifa wa CCM.

Kwa pamoja, wote walimpigia kura zote za ‘ndiyo’na hivyo kuhitimisha rasmi uenyekiti wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Sisi, Nipashe, tunampongeza Rais Magufuli kwa kutwaa jukumu la kukiongoza chama tawala, ikiwa ni takribani miezi minane sasa tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimrithi pia Rais mstaafu Kikwete.

Tunahitaji kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kutambua kuwa amejipambanua kuleta mabadiliko na kuhakikisha kuwa chama na serikali anayoiongoza vinaibadilisha Tanzania ambayo ina changamoto nyingi za kisiasa, kiuchumi, maadili na uwajibikaji.

Tunaona kuwa huu si wakati wa kukosoana na kulalamikiana bali kuweka mbele kazi na kulisaidia taifa ili kutimiza wajibu wa kumsaidia Rais kama alivyoahidi kuwa atawatumikia wananchi na serikali kwa kuwa yeye si mgeni wa chama na uongozi wa serikali tena ni muadilifu.

Rais akiwa amekabidhiwa kijiti na kuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano, ana nia njema ya kupunguza kama si kumaliza matatizo yaliyopo serikalini kama wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, kupitia wafanyakazi hewa, kukosekana uwajibikaji na matumizi mabaya ya ofisi na mamlaka huku wengine wakijisahau na kuendeleza ufisadi ndani ya ofisi za umma.

Rais Magufuli, ambaye ameahidi mambo mema, anakikuta chama na serikali vikiwa na changamoto nyingi, lakini imani ya Watanzania kwake inabaki kuwa ni kiongozi ambaye ni tinga tinga kwenye kazi na anayewajali na kuwafikiria wanyonge.

Mwenyekiti huyu wa CCM anastahili kuungwa mkono na kusaidiwa kwa kuwa ni kiongozi anayeionyesha Tanzania njia ya kufikia mafanikio.

Amefanya maamuzi na kufuatilia majukumu anayoyapanga, ana moyo wa kuliwezesha taifa kusomesha wanafunzi kupitia mpango wa elimu bora, kujenga miundombinu ya usafirishaji hasa bara bara na reli, kadhalika kuifanya nchi ijitegemee bila kuomba wahisani kwa kulipa kodi na kuwajibika kwenye matumizi ya umma.

Rais ameiamini na kuipa safu ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, kazi ya kuendelea kukiongoza chama na kushirikiana naye kukiongoza chama na serikali.

Tunatambua kuwa CCM imara itaipeleka nchi katika hali imara zaidi kiuchumi, kwani tunaamini kuwa chama tawala ndicho kinachounda serikali, uimara wa uchumi wa nchi utategemea serikali ya chama kilichoko madarakani.

Nasi tunawapongeza na kuwahimiza viongozi wa chama kuwa wasimuangushe Rais, bali waende na kasi hiyo hiyo ya hapa kazi tu, ili CCM na serikali yake itimize azma ya kuipaisha Tanzania kiuchumi, kisiasa na kiustawi wa jamii kama inavyokusudia.

Kama ambavyo amewaahidi Watanzania kuwa hatawaangusha, nasi tunampongeza na kumkumbusha kuwa ahadi ni deni, tunasubiri kuona akiipeleka serikali makao makuu Dodoma na pia kushirikiana na raia wote ili Tanzania ya Magufuli iifikishe Tanzania katika uchumi wa kati utakaoinua maisha ya wananchi maskini kuwa na maisha bora zaidi.

Habari Kubwa