Hongera Serikali kwa maboresho kwenye Uwanja wa Uhuru

10Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hongera Serikali kwa maboresho kwenye Uwanja wa Uhuru

KWANZA Nipashe tunaanza kwa kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuufanyia marekebisho Uwanja wa zamani wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru au Shamba la Bibi) ulioko jijini, Dar es Salaam.

Katika taarifa ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema kuwa marekebisho hayo yameigharimu serikali kiasi cha Sh. bilioni 12.

Hakika Uwanja wa Uhuru umebadilika kwa kiasi kikubwa hasa kuongezwa kwa majukwaa yaliyofunikwa pamoja na uboreshaji kwenye maeneo mengine ya uwanja huo ikiwamo vyoo na kuimarisha mfumo wa maji uwanjani hapo.

Uwanja huo umeanza kutumiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) Jumatano iliyopita kwa mchezo mmoja wa ligi uliozihusisha Simba dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.

Ni wazi fedha zilizotumikia kwa ajili ya marekebisho hayo ni za walipa kodi ambazo zingeweza kufanyiwa kitu kingine cha maendeleo lakini kutokana na Serikali kuthamini michezo ikizielekeza fedha kwenye ukarabati huo.

Sasa Uwanja huo ambao una nyasi bandia una uwezo wa kuingiza mashabiki 23,000.

Nipashe tunachukua fursa hii kuwakumbusha wanamichezo na wananchi kwa ujumla kuthamini na kuutunza uwanja huu ambao umeongeza idadi ya viwanja bora hapa nchini ukiacha Uwanja Mkuu wa Taifa, CCM Kirumba wa jijini Mwanza na Azam Complex ambao unamilikiwa na klabu ya Azam FC.

Tunaona tuwakumbushe wadau wa michezo juu ya utunzaji wa uwanja huo kutokana na kile ambacho tunakiona kwenye uwanja wa Taifa.

Tumeshuhudia mara nyingi vifaa mbalimbali kwenye uwanja wa Taifa vikiharibiwa kwa makusudi na mashabiki wa mpira bila kuona huruma fedha nyingi za walipa kodi zilizotumika kuujenga.

Koki za mabomba ya vyooni pamoja na masinki yake mara kwa mara vimekuwa vikiharibiwa kwenye uwanja wa taifa achilia mbali ung’oaji wa viti unaofanywa na mashabiki hasa pale timu zao zinapopata matokeo mabaya kwenye mechi za ligi au za kimataifa.

Si jukumu la Serikali peke yake kuhamasisha wananchi kuvitunza viwanja hivi ila pia ni jukumu la TFF na kila mdau kuhakikisha mchezo unachezeka kwa amani na uwanja unabaki katika hali ya usalama.

Utunzaji wa kitu unaanza kwa mtu mmoja mmoja, kama mashabiki tutakuwa na ustaarabu Nipashe inaamini hakutakuwa na usumbufu wa kufanyia marekebisho ya mara kwa mara katika viwanja vyetu ukiwemo uwanja huu uliozaliwa upya.

Lakini pamoja na hayo Nipashe tungepoenda kuwakumbusha jambo moja wenzetu wa TFF ambao ndio wanaadaaji na waratibu wa michezo ya ligi kuu inayofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Uwanja huu hauna taa za kutosha kuangaza sehemu yote ya uwanja hivyo iwe kwa siku za kazi au siku za mapumziko michezo kwenye uwanja huu inapaswa kuanza saa 10:00 jioni ili kuepuka giza kuanza kuingia huku mechi ikiwa bado haijamalizika.

Tumeshuhudia kwenye mchezo wa Jumatano iliyopita kati ya Ruvu Shooting na Simba ambao ulianza zaidi ya saa 10:30 jioni kujikuta mpaka zinafika dakika 10 kabla ya mpira kumalizika tayari giza lilianza kuingia na kuleta manung’uniko kwa baadhi ya mashabiki.

Suala la muda halina shida kwenye uwanja wa Taifa kutokana na miundo mbinu ya taa ambapo muda wote kuna kuwa na mwanga hata kama mpira ukaanza saa 10:30 lakini sio kwa Uwanja wa Uhuru.

Nipashe tunaona ni vyema kwa michezo yote kwenye uwanja wa Uhuru bila kuzingatia siku, ianze saa 10:00 badala ya saa 10:30 kwa siku za kazi.

Kwa mara nyingine tunaipongeza Serikali kwa uboreshaji wa uwanja huu wenye historia kubwa kwa taifa letu, na kwetu mashabiki tuelewe kuwea ni jukumu letu kuutunza ili kuepusha hasara zisizokuwa na msingi.

Habari Kubwa