Hongera TFF kuendesha michuano ya yosso U-15

15Jun 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Hongera TFF kuendesha michuano ya yosso U-15

WAKATI zikiwa zimebakia siku sita ili kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) huko Misri, tayari Tanzania imeanza maandalizi ya mashindano ya vijana ya umri chini ya miaka 17.

Timu ya Tanzania (Taifa Stars) ni moja kati ya mataifa 24 ambayo yatachuana katika fainali hizo zinazoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuwania kombe hilo linaloshikiliwa na Cameroon.

Taifa Stars inashiriki fainali hizo, baada ya kuzikosa kwa muda wa miaka 39, maana yake ilicheza mashindano hayo kwa mara ya mwisho mwaka 1980.

Lengo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuandaa mashindano ya U-15 ni kutaka kuanza kusaka vipaji vipya ambavyo vitapeperusha bendera ya nchi katika michuano mbalimbali katika siku za hivi karibuni.

Uamuzi wa kuandaa au kuendesha mashindano hayo chini ya Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia, yametokana na kikosi chake cha Taifa cha umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kufanya vibaya kwenye Fainali za Afrika (Afcon U1-7), ambazo zilifanyika hapa nchini Aprili mwaka huu.

Serengeti Boys ambayo ilionekana kuwatoa kimasomaso Watanzania, ilishindwa kufurukuta mbele ya timu nyingine kutoka Afrika Magharibi na hata majirani zao, Uganda.

Matokeo hayo mabaya, yaliifanya TFF ikae chini na kutathimini, jambo jipya la kufanya ili kuandaa wachezaji ambao watalelewa kwa muda mrefu, ambao ndio wataibeba nchi katika mashindano ya kimataifa.

Gazeti hili linawapongeza TFF kwa kuandaa mashindano hayo, ambayo yanashirikisha timu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Hii inaonyesha kuwa ahadi ya kuendeleza soka la vijana ambayo ilitolewa na Karia wakati ananadi sera zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo, inatekelezwa kwa vitendo.

Ni wazi kuwa katika soka hakuna njia ya mkato, ili nchi au klabu yako iweze kufanya vema katika mashindano ya ndani au ya kimataifa ni lazima, viongozi wakubali kuwekeza.

Ili Stars iweze kuwa na makali ni lazima, TFF na klabu kukubali kuwekeza katika soka la vijana na ndani ya miaka michache ijayo, matunda yataanza kuonekana kwa kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ambayo Tanzania itashiriki.

Hakuna nchi ambayo imepata mafanikio katika soka au mchezo wowote bila ya kuwekeza katika ngazi ya vijana pamoja na makocha, kwa sababu hivi ni vitu viwili vinavyoendana ili kufikia maendeleo.

Nipashe inawapongeza TFF kwa kukubali kuanza kuwajenga wachezaji chipukizi ili ndoto za kubeba makombe mbalimbali ziweze kutimia, pia mikoa yote ambayo imeleta wachezaji ambao umri wao ni mdogo kama walivyoelekezwa.

Kuendesha mashindano ya vijana au ligi za wanawake ni gharama, kwa sababu hakuna kampuni ambazo zinajitokeza kudhamini michuano hiyo, lakini ni ukweli kuwa, mashindano ya vijana ndiyo yanayovumbua vipaji na yanayojenga wachezaji kwa kupitia mifumo sahihi.

Watanzania tunatakiwa tubadilike kwa kukubali kuwekeza katika michezo ya vijana, na hapo tutatarajia kuwa na wachezaji wenye viwango ambao watapeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa na jina la "Kichwa cha Mwenzawazimu" litabakia kuwa historia.

Habari Kubwa