Hongera waliofanya vizuri kidato cha sita lakini safari bado mbichi

16Jul 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Hongera waliofanya vizuri kidato cha sita lakini safari bado mbichi

BARAZA la Taifa la Mitihani (Necta), jana lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Mei hadi Juni, mwaka huu, huku yakionyesha kuwa ufaulu umeshuka kulinganisha na yale ya mwaka uliopita.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Zanzibar na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Musonde, ufaulu wa mwaka huu umekuwa asilimia 96.06 kulinganisha na asilimia 97.94 ya mwaka jana.

Licha ya kushuka kwa ufaulu huo kwa kiwango kidogo, matokeo hayo yanaonyesha kuwa wasichana wameng’aras zaidi kulinganisha na wavulana.

Mitihani hiyo iliusisha watahiniwa 73,692 kati ya 75,116 wakiwamo 63,055 wa shule na 12,061 wa kujitegemea. Watahiniwa 1,424 hawakufanya mitihani hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa upande wa ufaulu, watahiniwa 70,552 sawa na asilimia 96.06 wamefaulu wakiwamo wasichana ni 27,577 (asilimia 97.21) na wavulana 42,975 sawa na asilimia 95.34 katika kundi hilo.

Aidha, katika ufaulu huo, watahimiwa 58,556 wa shule, sawa na asilimia 93.72 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu. Katika waliofaulu hao, wamo wasichana 22,909 (na asilimia 94.07) na wavulana 35,647 ambao ni asilimia 93.49.

Kwa ujumla, matokeo hayo yameonyesha kuwa shule maarufu za binafsi kama vile Feza Boys na Girls, Marian Boys na Girls, St. Mary’s Mazinde Juu, Patrick Mission, St. Joseph Cathedral na St. Maria Goreti zimeibuka vinara katika matokeo hayo.

Pia shule kongwe za serikali kama vile Mzumbe, Kibaha, Ilboru, Weruweru, Umbwe, Kilakala na Tabora Wasichana, zimefanya vizuri kwa kutoa wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri huku zingine maarufu, ikiwamo Azania zikifanya vibaya.

Hakika hayo ni matokeo yanayoonyesha uhalisia wa kila shule ilivyojiandaa kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wake wanafaulu. Kwa maneno mengine, matokeo hayo yanaonyesha nini kila shule imevuna kutokana na kile ilichopanda.

Kwa upande mwingine, matokeo hayo yanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwa mitihani ijayo kwa kila shule ili kufanya vizuri zaidi kwa zile zilizofanya vibaya na zilizofanya vizuri, kuendelea kusimama katika nafasi hizo bora.

Kutokana na matokeo hayo, tunawapongeza wanafunzi wote waliofaulu ambao wana sifa za kujiunga na masomo ya elimu ya juu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu za ndani na nje ya nchi.
 
Licha ya pongezi hizo, ni vyema wanafunzi hao waliofaulu na kupata nafasi za masomo ya juu zaidi, wasibweteke na kiwango cha ufaulu wao bali iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi katika masomo ya shahada ya kitaaluma.

Lakini kwa wale ambao hawakufanya vizuri, watambue kuwa huo si mwisho wa safari yao kielimu bali watumie kama changamoto ya kufanya vizuri kwenye fani nyingine na maisha kwa ujumla.

Tunasema kufaulu huko ni moja ya hatua muhimu katika safari ya kielimu kwa sababu kwa miaka mingi tumeshuhudia wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sekondari hawaendelezi ari hiyo na badala yake wanafeli na kutokuendelea na masomo ya ngazi za shahada au stashahada za juu.

Kwa mantiki hiyo, wahitimu hao wa kidato cha sita wanapaswa kutambua kuwa mafanikio hayo ni sawa na tiketi ya kuingia vyuo vikuu lakini wakifika huko ni lazima waonyeshe uwezo zaidi ili kuuthibitishia umma kuwa hawajafanikiwa kupata nafasi hizo kwa kubahatisha.